Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rumbek 98 FM mnachohitaji sasa ni jua tu kusikika hewani kila siku- UNMISS

Paneli za sola zikiwa dukani. Paneli hizi ni muarobaini kwenye maeneo yasiyo na umeme unaolishwa kwa kutumia nishati nyingine.
Mohamed Nasser
Paneli za sola zikiwa dukani. Paneli hizi ni muarobaini kwenye maeneo yasiyo na umeme unaolishwa kwa kutumia nishati nyingine.

Rumbek 98 FM mnachohitaji sasa ni jua tu kusikika hewani kila siku- UNMISS

Utamaduni na Elimu

Wananchi wa Rumbek nchini Sudan Kusini, sasa watahabarika kutwa nzima kila siku, tena kwa kupitia lugha mbalimbali ikiwemo lugha ya mama Dinka, Kiarabu na Kiingereza baada ya Radio pekee ya jamii inayoendeshwa na serikali ya Rumbek 98FM kupigwa jeki na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS. 

UNMISS ambayo kwa muda imekuwa ikisikia kilio kutoka kwa viongozi wa serikali wa Rumbek na wananchi cha kushindwa kupata taarifa muhimu kutokana na changamoto za nishati ya kuendesha matangazo ya kituo cha Rumbek FM , ambapo mara kadhaa genereta inaishiwa mafuta na kulazimika kufunga matangazo wakati mwingine kwa siku kadhaa, leo  imeamua kuwafuta machozi, kwa kutoa msaada wa paneli za sola ambazo zitaiwezesha Radio hiyo inayotangaza kwa lugha mbalimbali kuwa hewani kila siku.

Kwa mujibu wa UNMISS sasa wanachohitaji ni jua tu lisilo na gharama yoyote kutimiza ndoto yao. Kwa furaha kubwa Maria Amakom mwandishi habari wa kituo hicho amesema “sasa tutaweza kupanua wigo wa matangazo yetu kwa lugha tofauti na kujumuisha vipindi ambayo vitawavutia vijana na wanawake na tutakuwa na muda wa kutosha kufikisha ujumbe wa amani.”

Na hayo ndio matarajio ya UNMISS pia, kuwa mbali ya kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha, Rumbek FM 98 itakuwa na jukumu kubwa la kuchagiza suluhu ya migogoro ya kikabila na kufanya mijadala itakayojikita katika mazungumzo ya amani, na masuala mengine yanayozitatiza jamii za Rumbek kwenye jimbo la Western Lakes.

Radio ni mkombozi kwa watu wengi kwa kuwa  huwezesha kupata habari kwa kina kama hapa inavyoonekana kwa wakazi wa Sangari Jamhuri ya Afrika ya kati wakisikiliza Radio Lego Tila Ouaka( Sauti ya Ouaka) radio ya jamii inawaleta pamoja waislamu na wakristo
Picha ya OCHA/Gemma Cortes
Radio ni mkombozi kwa watu wengi kwa kuwa huwezesha kupata habari kwa kina kama hapa inavyoonekana kwa wakazi wa Sangari Jamhuri ya Afrika ya kati wakisikiliza Radio Lego Tila Ouaka( Sauti ya Ouaka) radio ya jamii inawaleta pamoja waislamu na wakristo

Akiishukuru UNMISS kwa msaada huo gavana wa Western Lakes, Lois Agum Ruben amesema chaguo la watu wa Rumbek kuishia kusikiliza sauti za ndege wa porini wakiimba baada ya matangazo kutatika, sasa litakishwa na anafurahi sana hatimaye kilio chao kimesikika akisema kwani “Leo ndoto zetu zimetimia , na hii itatupa fursa ya kusikiliza sauti za jamii yetu, na sisi kama serikali tutawafikia watu wetu kwa urahisi kupitia Radio hii”

Mkuu wa UNMISS ofisi ya Rumbek Kwame Dwamena-Abaogye amesema,  msaada huo wa paneli za sola zilizoghariimu dola 48,000 ni sehemu ya miradi yenye lengo la kuleta maendelo kwa jamii kupitia gharama nafuu,. Ameongeza kuwa endapo zitatunzwa vizuri basi Rumbek FM 98 itawaweza kuzitumia paneli hizo kutangaza saa 24 kwa miaka 20 ijayo, na ameahidi  miradi mingine ya kunufaisha jamii kutoka Umoja wa Mataifa itafuata.