Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ya apu kiganjani yasaidia wanawake kumiliki ardhi Tanzania

Hiki ni kipengele kiitwacho Mwanamke na Ardhi kilichoko kwenye Apu ya Sheria Kiganjani. Kipengele hiki kimebuniwa na Dkt. Monica Magoke Mhoja, Mkurugenzi wa LANDESA barani AFrika baada ya kupatiwa ufadhili na Bertha Foundation.
Bertha Foundation Video
Hiki ni kipengele kiitwacho Mwanamke na Ardhi kilichoko kwenye Apu ya Sheria Kiganjani. Kipengele hiki kimebuniwa na Dkt. Monica Magoke Mhoja, Mkurugenzi wa LANDESA barani AFrika baada ya kupatiwa ufadhili na Bertha Foundation.

Teknolojia ya apu kiganjani yasaidia wanawake kumiliki ardhi Tanzania

Wanawake

Wakati mkutano wa 67 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake duniani ukiingia siku ya pili hii leo maudhui yakiwa matumizi ya teknolojia kumkwamua mwanamke, mmoja wa washiriki katika mkutano huo ameieleza Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, HABARI ZA UN ni kwa vipi ubunifu wa kwenye simu umesaidia kuwarejeshea haki ya ardhi wanawake hasa wale walio pembezoni nchini Tanzania, mathalani wajane.

Dkt. Monica Mhoja, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki ya ardhi kwa wanawake, LANDESA, barani Afrika amesema yeye na wadau walifikia hatua hiyo baada ya kuona kuwa Tanzania, kama ilivyo katika baadhi ya mataifa mengine sheria za ardhi zinampatia fursa mwanamke kumiliki na kutumia ardhi kama mwanaume, lakini changamoto ni utekelezaji.

Tweet URL

Sheria kiganjani na Mwanamke na Ardhi

LANDESA barani Afrika lilianzisha kampeni iitwayo Linda Ardhi ya Mwanamke ambayo kitaifa ilianzia Tanzania. Na ili kufikia hata wanawake wa kijijini, LANDESA ambayo ndio Sekretarieti ya kampeni hiyo ya Linda Ardhi ya Mwanamke kwa kushirikiana na wadau wa kampeni Sheria Kiganjani walio na apu ya kutoa huduma mbalimbali, nikabuni kupitia ufadhili wa taasisi ya Bertha Foundation sehemu ya huduma ndani ya apu ya Sheria Kiganjani kipengele cha kutoa huduma kuhusu masuala ya ardhi na kipengele hicho nilikiita Mwanamke na Ardhi,” amesema Dkt. Mhoja akihojiwa na Assumpta Massoi wa Habari za UN jijini New York, Marekani.

Je Mwanamke na Ardhi inafanyaje kazi?

Huduma hiyo inapatikana kwa njia ya simu janja, lakini kutokana na kwamba si wanawake wengi vijijini wana simu janja hatua zaidi ilichukuliwa.

“Kwa hicho tulichofanya tulichagua mkoa wa Pwani na pia mkoa wa Dar es salaam hususan maeneo ya pembezoni ya wilaya ya Kinondoni. Tulimulika zaidi wajane. Tulichukua Chama cha Wajane Tanzania ili kupata watu wawili kwenye chama wanaoweza kusaidia wajane. Na vijijini tulikwenda vijiji vya Chamgoi na Ngarambe wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.”

Tulipata viongozi wanawake na wanaume, mfano wenyeviti wa vijiji, watendaji, mabwana shamba, maafisa maendeleo na tukawaita kama wahamasishaji.

Viongozi hao walifundishwa sheria za ardhi na jinsi ya kutumia kipengele cha Mwanamke na Ardhi kwenye apu ya Sheria Kiganjani.

Muundo wake

Kwa sababu vijijiini wakati mwingine hata kupata mtandao ni shida, wale waliopatiwa mafunzo waliwekewa katika simu janga Apu ya Sheria Kiganjani ikiwe na kipengele cha Mwanamkena Ardhi.

Mhusika anajisajili na hivyo ataweza kukusanya taarifa kutoka kwa wanawake wanaokabiliwa na changamoto za ardhi, miradhi, watoto yatima au masuala mengine kama ukatili wa kijinsia.

“Mimi niliyeko mjini nikifungua kompyuta mpakato yangu au mwanasheria wa Sheria Kiganjani akifungua apu yake ataona mtendaji wa kijiji cha Ngarambe leo ameweza kusajili wanawake wenye matatizo ya mirathi au watoto yatima! Na ndani yake tutaona ni namna gani amewasaidi. Ndani ya apu hiyo, Sheria Kiganjani imeweka fursa ya msaidizi huyo wa sheria kijijini kuweza kupiga simu saa 24 iwapo kuna kitu amekwama. Hivyo anapatiwa msaada zaidi,”amesema Dkt. Mhoja.

Dkt. Monica Magoke Mhoja akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando ya CSW67 jijini New York, Marekani kuhusu kipengele cha apu alichobuni kiitwacho Mwanamke na ARdhi ambacho kinasaidia wanawake wa pembezoni kupata haki zao za ardhi.
UN / Assumpta Massoi
Dkt. Monica Magoke Mhoja akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando ya CSW67 jijini New York, Marekani kuhusu kipengele cha apu alichobuni kiitwacho Mwanamke na ARdhi ambacho kinasaidia wanawake wa pembezoni kupata haki zao za ardhi.

Mwanamke na Ardhi imekuwa mkombozi

Kwa mujibu wa Dkt Mhoja tayari kuna simulizi za mafanikio akitoa mfano wa mwanamke mmoja aitwaye Doto mkazi wa mkoa wa Pwani ambaye baada ya kufikiwa na wasaidizi wa sheria kupitia Mwanamke na Ardhi ameweza kupata  umiliki wa ardhi aliyokuwa hana fursa nayo.

“Doto baada ya kupata ushauri wa kisheria kupitia ubunifu wa hii teknolojia akagundua kwamba kumbe anaweza kukusanya wanawake wenzake wakawa na umoja wakaenda kupata fedha za mkopo kwenye kata na wakaenda kuomba kijijini wakapewa ardhi. Sasa hivi wana vikundi vya kulima pamoja na mashamba waliyopata kijijini baada ya kugundua kuwa sheria ya ardhi ya kijiji inawapa haki,” amesema Dkt. Mhoja akiongeza kuwa awali walidhani sheria inawapa haki wanaume pekee.

Dotto hivi sasa ana ardhi yake analima ufuta, ana ardhi analima na familia na ana ardhi ya kikundi na ameweza kulipa ada ya shule ya mtoto wake, mtoto ambaye amehitimu shule na kupata daraja la kwanza.

Wanasema Mwanamke na Ardhi imekuwa mkombozi wa kuwatoa kwenye umaskini.

Kwa mujibu wa Dkt .Monica, wakati wa janga la COVID-19, aligundua kuwa apu hiyo inaweza kutumika kwa mawasiliano hivyo wakaiboresha ili iweze kutumika kutuma ujumbe wa kuondoa wasiwasi kwa wakazi wa vijijini.

Wangapi wamenufaika na Mwanamke na Ardhi

Wakati wa usaidizi kutoka Bertha Foundation ,Dkt. Monica aliweza kupatia wasaidizi wa kisheria 35 mafunzo ya matumizi ya hicho kipengele cha Mwanamke na Ardhi, halikadhalika wajane zaidi ya 50 wamehalalishiwa maeneo yao ya ardhi.

Kupitia kipengele hicho pia nilisoma ya kwamba vikundi vitatu vimesaidiwa kupata ardhi baada ya kupata elimu na kujua kuwa wanaweza kupata ardhi. Na vikundi hivyo vitatu navyo vimeweza kufikia wanawake takribani 2,000 na kuwapa elimu. Hii imetokana na teknolojia ya kiganjani ambayo imekuwa sehemu ya kuwajengea uwezo kwani ardhi si ya wanaume tu au si ya kaka yang utu.”