Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW67 yafungua rasmi pazia kwa wito wa kuongeza wanawake kwenye sayansi na teknolojia

Kikao cha 67 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW67 kimeanza rasmi hii leo mjini New York Marekani
UN Photo/Manuel Elías
Kikao cha 67 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW67 kimeanza rasmi hii leo mjini New York Marekani

CSW67 yafungua rasmi pazia kwa wito wa kuongeza wanawake kwenye sayansi na teknolojia

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mfumo wa kidunia haufanyi kazi na mfumo dume unasukuma nyuma maendeleo ya wanawake hivyo ni lazima juhudi ziendelee kuhakikisha maslahi na maendeleo ya wanawake yanafikiwa duniani kote.

Guterres ameyasema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa 67 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW ulioanza leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

“Mkutano wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake ni moja ya matukio muhimu ya kila mwaka katika Umoja wa Mataifa. Unachukua juhudi muhimu na kubwa zaidi katika wakati huu ambao hali za wanawake zinanyanyaswa, kutishiwa, na kukiukwa kote ulimwenguni.” Amesema Guterres

Maendeleo ya karne yanapotea mbele ya macho yetu

“Kuanzia Ukraine mpaka ukanda wa Sahel hali za wanawake zinaendelea kuwa mbaya” amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa na kutaja unyanyasi dhidi ya wanawake unaofanyika nchini Afghanistan na hata baadhi ya nchi ambazo wanawake na wasichana wanaenda wanatembea au kwenda shule huku wakiwa na wasiwasi wa kuweza kutekwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Mengine ni pengo la usawa wa kijinsia linaendelea kuongezeka, vifo wakati wa ujauzito au wakati wa kujifungua ambavyo vingeweza kuzuilia pamoja na changamoto zilizo chochewa na COVID-19 ni baadhi ya masuala yanayorudisha nyuma juhudi za kuwakomboa wanawake.

Mfumo dume unapigana nasi

Guterres amesema ingawa mfumo dume unapigana na juhudi za kuendeleza maendeleo ya wanawake lakini ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anapigana nao ili kufikia maendeleo kamili ya wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kikao cha 67 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kikao cha 67 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani

“Niko hapa kusema kwa sauti kubwa na kwa uwaz: Umoja wa Mataifa unasimama na wanawake na wasichana kila mahali.” Amesema Guterres na kutaja baadhi ya juhudi zinazofanywa ikiwa ni pamoja na safari ya hivi karibuni ya Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohammed na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN WOMEN Sima Bahous nchini Afghanistan walipoenda kuzungumza na utawala wa Taliban kuhusu haki za wanawake na wasichana nchini humo baada ya kupigwa marufuku kufanya kazi na shule.

Lengo la mwaka huu la mkutano huo ni kuhakikisha pengo la teknolojia linapunguzwa, wasichana na wanawake wanajumuishwa kwenye masuala ya teknolojia.

Hesabu ipo wazi kabisa bila kuwashirikisha jamii yote dunia itafaidi nusu tu ya uwezo wake kwakuwa wengine watakuwa wameachwa nyuma kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.

“Watu bilioni tatu bado hawajaunganishwa kwenye huduma ya intaneti na wengi wao ni wanawake na wasichana katika nchi zinazo endelea. Katika nchi zenye uchumi duni 19% ya wanawake ndio wameunganishwa mtandaoni. Ulimwenguni kote wasichana na wanawake ni theluthi moja tu ya wanawafunzi wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandishi na hisabati.”

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kukuza michango ya wanawake kwenye sayansi, teknolojia na uvumbuzi sio kitendo cha hisani au neema kwa wanawake. Inafaidi kila mtu kwani wanawake wanapopata huduma za matibabu kupitia mtandaoni, familia zao na jamii zinapata afya.

Tunaweza kupata nuru baadae kwa kuwekeza kwenye AI sasa

Kauli hii ya Guterres imeungwa mkono na Rais wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi, ambaye naye alizungumza baada ya Katibu Mkuu na kusema teknolojia mpya iwapo itatumika vizuri itasaidia kuleta usawa na kubadili mambo mengi.

“Wajasiriamali wachanga wanatengeneza programu mpya za kulinda wanawake na wasichana kutokana na vitendo vya ukatili. kujifunza mtandaoni katika baadhi ya maeneo kunapunguza pengo la usawa kijinsia, kuwaandaa wanawake kwaajili ya kupata kazi kidijitali na kuwaunganisha wanawake na fursa za kufanya kazi.” Amesema Kőrösi

Ameongeza kuwa matumizi ya akili bandia AI ambayo yataimarisha uchumi wetu kesho yanaweza kubuniwa kwa njia ambazo zinafuta ubaguzi wa kijinsia ulioko leo.

“Kwa kukabiliana na mitindo ambayo inazuia wasichana kuchagua kusoma na hatimaye kupata kazi kwenye eneo la sayansi, hisabati na teknolojia STEM, tunaweza kufanya kazi kubadilisha mawazo na kuongeza utofauti wa mawazo katika maeneo yetu ya kazi.” Akisema Mkuu huyo wa UNGA77

Hali ya kidijitali ya wanawake na wasichana katika ulimwengu wa sasa

Bi. Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji  wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women akizungumza katika mkutano huu wa 67 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW67 anasema,

"Aina mpya ya umaskini sasa inaikabili dunia, umaskini ambao unawaengua wanawake na wasichana kwa hali inayotia sana uchungu, na umaskini huo ni ule wa kidijitali.  Mgawanyiko wa kidijitali umekuwa taswira mpya ya ukosefu wa usawa wa kijinsia, ambao umesababisha wanawake na wasichana kusukumwa nyuma kama tunavyoshuhudia katika ulimwengu wa leo. Ndio maana mkutano huu wa 67 wa kamisheni ya wanawake umekuwa ni wa wakati muafaka na muhimu zaidi kutimiza kazi yake”.