Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miongo zaidi ya miwili ya azimio 1325, bado wanawake wanaenguliwa kwenye mazungumzo ya amani

Verónica Nataniel Macamo Dlhovo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji akiongoza kikao cha Baraza la Usalama la UN hii leo lililokutana kujadili wanawake, amani na usalama.Msumbiji inashikilia kiti cha Urais wa Baraza kwa mwezi huu wa Machi.
UN /Manuel Elias
Verónica Nataniel Macamo Dlhovo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji akiongoza kikao cha Baraza la Usalama la UN hii leo lililokutana kujadili wanawake, amani na usalama.Msumbiji inashikilia kiti cha Urais wa Baraza kwa mwezi huu wa Machi.

Miongo zaidi ya miwili ya azimio 1325, bado wanawake wanaenguliwa kwenye mazungumzo ya amani

Amani na Usalama

Ingawa kuna mambo ya kihistoria yametokea kwenye masuala ya usawa kijinsia katika zaidi ya miaka 20 ya azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, bado hakuna mabadiliko makubwa katika meza za mazungumzo ya amani au hatua kwa wale wanaotekelezza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women, Sima Sami Bahous hii leo jijini New York, Marekani.

Ametoa kauli hiyo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana leo kujadili Wanawake, Amani na Usalama, wakati huu ambapo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kunafanyika mkutano wa 67 wa Hali ya Wanawake Duniani, CSW67.

Kikao hicho kiliongozwa na Verónica Nataniel Macamo Dlhovo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji  kwa kuwa Msumbiji inashikilia kiti cha Urais wa Baraza kwa mwezi huu wa Machi.

“Nakumbuka ziara yangu nchini Afghanistan wiki chache tu zilizopita. Tangu wakati huo, Watalibani wametangaza vizuizi zaidi na wamewasweka ndani wanaharakati wengi zaidi, akiwemo mtetezi wa haki za wanawake Narges Sadat na Ismail Meshaal ambaye ni Profesa wa Chuo Kikuu kwa ujasiri wao wa kuonesha mshikamano na wanawake nchini Afghanistan na haki yao ya kupata elimu,” amesema Bi. Bahaous.

Ukatili wa kingono unazidi kushamiri kwenye mizozo

Ametaja pia ukatili wa kingono umetekelezwa kwa kiwango cha juu nchini Ethiopia. Ndo za utotoni zimeongezeka kwa asilimia 51 ndani ya mwaka mmoja wa mzozo. Katika vituo vya afya, mashirika ya kutoa misaada na yale ya haki za binadamu yanaendelea kuripoti ukatili wa kingono.

Zaidi ya hayo amesema kuwa hali ya wanawake imetekwa. Vipengele vya teknolojia, kama vile mitandao ya kijamii vina dhima muhimu katika kushirikisha taarifa na kuonesha usaidizi, lakini wakati huo huo vinasababisha uharibifu kwa kusambaza taarifa za uongo na kuchochea ubaguzi wa kijinsia.

Sima Sami Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women (mwenye blauzi nyekundu) akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kujadili Wanawake, Amani na Usalama 7 Machi 2023
UN /Manuel Elias
Sima Sami Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women (mwenye blauzi nyekundu) akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kujadili Wanawake, Amani na Usalama 7 Machi 2023

Bi. Bahous amesisitiza “ni muhimu serikali na kampuni binafsi zikashirikiana kuchochea teknolojia kama kiwezeshaji cha maendeleo.”

Amesema katika mazingira ya sasa ya mizozo kama huko Ukraine, amani ndio jawabu huku wanawake wakishiriki katika mchakato huo.

Amesisitiza hatuwezi kutarajia mwaka 2025 uwe tofauti iwapo hatua nyingi tunazochukua zitaendelea kuwa ni mafunzo, uhamasishaji, utoaji mwongozo, uwezeshaji, kuendesha matukio moja baada ya lingine kuhusu ushiriki wa wanawake badal ya kutekeleza maamuzi tuliyopitisha katika kila mchakato wa maamuzi ambayo tuna mamlaka nayo.

Wanawake ndio nguzo kwenye kusaka jamaa waliopotea

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, Mirjana Spoljaric Egger,katika hotuba yake akasema kila siku shirika lao linashuhudia dhima muhimu ambayo wanaweza wanatekeleza katika kulinda na kuongoza familia na jamii.  Mathalani katika kuhamasisha na kusaka jamaa zao waliopotea.

Amesema ICRC inaelewa vema kuwa hatua za kiutu ambazo zinashindwa kuhusisha kipengele cha jinsia ziko katika nafasi kubwa zaidi za kuimarisha ubaguzi wa kijinsia au aina nyingine ya ukatili.

Hivyo amesema, “serikali lazima zihakikishe kuwa katazo la dhahiri la ukatili wa kingono kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu linajumuishwa katika sheria ya kimataifa na mafunzo ya kijeshi.”

Muungano wa Afrika uliwakilishwa na Mjumbe wake Maalum wa Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama Bineta Diop.

“Tunahitaji kuchukua hatua zaidi hasa kwa kuzuia ukiukwaji wa haki na kusaidia manusura ili kujenga upya maisha kupitia program za kiuchumi, kijamii na kisaikolojia. Tunahitaji hatua za dharura kutokomeza ukwepaji sheria na wahusika wafikishwe mbele ya sheria,” amesema Bi. Diop

Hawa Games Dahab Gabjenda ana uzoefu mkubwa kama mtaalamu wa jinsia, amefanya kazi katika uwezeshaji wa wanawake, maendeleo, misaada ya kibinadamu na mipango ya kujenga amani.
Maimana El Hassan
Hawa Games Dahab Gabjenda ana uzoefu mkubwa kama mtaalamu wa jinsia, amefanya kazi katika uwezeshaji wa wanawake, maendeleo, misaada ya kibinadamu na mipango ya kujenga amani.

Michakato ya amani bila wanawake ni sawa na kutazama picha kwa jicho moja

Naye Leymah R. Gbowee, mshindi wa mwaka 2011 wa Tuzo ya Amani ya Nobel alitumia mkutano huo kutaka kila mdau duniani aone wanawakem amani na usalama kama sehemu moja ya kufanikisha ajenda ya amani na usalama duniani. Tutaendelea kusaka amani bila mafanikio yoyote iwapo wanawake hawatakuwa sehemu ya wanaoshiriki majadiliano mezani.

Ameongeza kuwa anaamini kwa dhati kwamba kujaribu kufanyika kazi ajenad ya amani na usalama bila kujumuisha wanawake ni sawa na kujaribu kutazama picha huku jicho moja limefungwa.

Azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2000 likitaka pande kinzani kwenye mizozo kuzuia ukiukwaji wa haki za wanawake, kusaidia ushiriki wa wanawake kwenye mashauriano ya kisasa na ushiriki wao kwenye michakato ya ujenzi wa nchi zao baada ya mizozo na kulinda wanawake na watoto wa kike dhidi ya ukatili wa kingono.