Guterres: Kuwaacha watu katika kambi ya Al-Hol kutajenga chuki kwa vizazi vijavyo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameipongeza Iraq kwa kuwarejesha nyumbani raia wake kutoka kambi ya Al- Hol iliyoko kaskazini mashariki mwa Syria iliyokuwa ikiwashikilia watu wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na wanamgambo wa kikundi cha ISIL, na kuzitaka serikali zingine "kuwajibika na kuchukua hatua".
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara yake katika kituo cha ukarabati cha Jeddah kilichoko kaskazini mwa Iraq, ambako alikutana na watu waliorejea kutoka katika kambi ya Al-Hol, ambayo wakazi wake wengi ni wanawake na watoto walio na umri wa chini ya miaka 12.
"Iraq inadhihirisha kwa dhamira kubwa kwamba uwajibikaji wa kuwarejesha watu unawezekana, kwa kutafuta suluhisho zenye heshima zilizo ainishwa kwenye kanuni za uwajibikaji zinazoingiliana. Na hili limewezekana na mimi nimeshuhudia leo,” alisema.
Katibu Mkuu Guterres ambaye ni Kamishna Mkuu wa zamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulika na wakimbizi UNHCR ametembelea kambi zote ulimwenguni, alikuwa na hakika kwamba Al-Hol ni "kambi mbaya zaidi katika ulimwengu wa leo", akibainisha kuwa watu wamekwama huko kwa miaka na katika hali mbaya zaidi.
Alisema wafungwa wamekuwa wakinyimwa haki zao, na wako katika mazingira magumu na kutengwa, na kubaki katika hali ya kukata tamaa isiyo na mwisho.
"Wanastahili njia ya kutoka. Hili ni suala la adabu na huruma ya binadamu, na ni suala la usalama," alisema, "Kwa sababu kadiri tunavyoruhusu hali hii isiyoweza kuepukika kuongezeka, ndivyo chuki na kukata tamaa kutaongezeka, na hatari zaidi kwa usalama na utulivu. Ni lazima tuzuie urithi wa pambano la jana lisichochee mzozo wa kesho.”
UN chief @antonioguterres in in northern #Iraq where he visited returnees repatriated from #Syria's notorious Al-Hol camp https://t.co/6UCkQKlDiQ
UN_News_Centre
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameipongeza Serikali ya Iraq kwa juhudi zake, alizoziita "mfano kwa ulimwengu", ingawa anatambua kuwa kurejea nyumbani ni suala gumu sana, lenye changamoto na nyeti.
Alitoa wito kwa nchi ambazo zina raia katika kambi ya Al-Hol na kwingineko "kuongeza juhudi zao" za kuelekea kuwarejesha kwa usalama na kwa heshima watu walioko kambini hapo.
"Wanahitaji kufuata mfano wa Iraq", alisema Bw. Guterres. "Nchi zote zilizo na raia wao katika Al-Hol lazima zifanye vivyo hivyo, katika urejeshaji wa heshima kulingana na sheria zinazotumika za kimataifa, na kwa watoto, kwa kuongozwa na kanuni za masilahi bora ya watoto."
Bw. Guterres alisema watu waliorejea aliokutana nao katika kituo cha ukarabati wanataka kujumuika katika jamii zao.
Amehimiza mamlaka ya Iraq kuendelea kufanya kazi kuelekea ujumuishaji wao wa kijamii, akibainisha kuwa wengi wako chini ya umri wa miaka 18.
Katibu Mkuu alisisitiza kujitolea kwa Umoja wa Mataifa na kuunga mkono kile alichokiita "juhudi hii muhimu".