Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata kama nakula vitunguu, wangalikuwa wazima nisingalikuwa na hofu- Ronia

Mwanamke wa kabila la Yazid akizungumza na Angelina Jolie, mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.
UNHCR/A. McConnell
Mwanamke wa kabila la Yazid akizungumza na Angelina Jolie, mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Hata kama nakula vitunguu, wangalikuwa wazima nisingalikuwa na hofu- Ronia

Msaada wa Kibinadamu

Mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Angelina Jolie, amerejea tena nchini Iraq na kushuhudia jinsi wakimbizi kutoka Syria wanavyohaha kuishi ikiwemo kulea watoto wao wenye mahitaji maalum.

Ndani ya makazi ya wakimbizi kwenye kambi ya Domiz, kaskazini mwa Iraq, Ronia, mama wa watoto watano na mkimbizi kutoka Syria akijaribu angalau kuwapa raha watoto wake kwa kuwabebesha ndani ya bembea iliyofungwa ndani ya chumba chao.

Ronia ambaye ni mjane kutoka kabila la wakurdi anasema..

“Ingalikuwa naishi bila chochote, kwa kula mkate na vitunguu na wanangu si wagonjwa, hiyo ingalikuwa sawa. Lakini magonjwa yao yametugharimu sana.”

Ronia analea watoto watano yeye peke yake. Wawili kati yao wana tatizo la damu ambalo linadumaza makuzi  yao na wanaweza kufariki dunia.

“Mume wangu aliugua ugonjwa huu na alifariki dunia kwani hapa hakukuwepo na tiba.”

Punde wanapata ugeni, ni mjumbe maalum wa UNHCR, Angelina Jolie anaketi na kuzungumza nao akimweleza kuwa ni mapito makubwa sana kuweza kulea familia yake.

Ronia anatakiwa kwenda hospitali kila wiki ili watoto wake wawili waweze kuongezewa damu.

“Angalau ameweza kuwa na nyumba yenye upendo na watoto wanatabasamu licha ya yote haya. Ni pongezi kubwa kwake.”

Hofu ya Ronia hivi sasa ni penginepo watoto wake hao wawili watafariki dunia kwa kuwa hawapati matibabu kama ambayo walikuwa wanapata nchini Iraq.

Tangu aanze kushirikiana na UNHCR mwaka 2001, Bi. Jolie amefanya ziara 61 ambapo hii ya Domiz ni ya tatu ilhali Iraq kwa ujumla ametembela mara 5.

TAGS: Angelina Jolie, UNHCR, Domiz, Iraq,