Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Syria waendelea kumiminika Iraq, UHCR yaongeza msaada

Mtoto katika kituo cha utambuzi kwenye kijiji cha Sahel nchini Iraq ambako wasyria 182 wamevuka mpaka na kuingia kufuatia mapigano mapya kaskazini-mashariki mwa nchi yao. Wakimbizi hawa wanapata msaada kutoka IOM. (Oktoba 2019)
IOM/Vanessa Okoth-Obbo
Mtoto katika kituo cha utambuzi kwenye kijiji cha Sahel nchini Iraq ambako wasyria 182 wamevuka mpaka na kuingia kufuatia mapigano mapya kaskazini-mashariki mwa nchi yao. Wakimbizi hawa wanapata msaada kutoka IOM. (Oktoba 2019)

Wakimbizi wa Syria waendelea kumiminika Iraq, UHCR yaongeza msaada

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakimbizi wa Syria zaidi ya 12,000 wamesaka hifadhi katika nchi jirani ya Iraq tangu kuzuka wimbi kubwa la wakimbizi siku nne zilizopita kwa mujibu wa timu ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo kupitia msemaji wake Andrej Mahecic mjini Geneva Uswis inasema idadi ya wakimbizi waliopo sasa katika kambi mpuya iliyofunguliwa hivi karibuni ya Bardarash ina wakimbizi zaidi ya 1,000 na wengine zaidi ya 800 hivi sasa wamepewa malazi katika kituo cha muda cha Gawilan . Maeneo yote mawili yako takriban kilometa 150 eneo la Mashariki mwa mpaka baina ya Iraq na Syria. Mahecic amesema “UNHCR na mamlaka ya Iraq wanashirikiana kuwaunganisha wakimbizi walio kambini na familia zao ambazo zinaishi katika jimbo la Kurdistan (KRI)nchini Iraq”.

Ameongeza kuwa pia UNHCR inasaidia juhudi zinazofanywa na malaka ya KRI na kufanya kazi kwa karibu kuandaa maeneo mengine tayari kupokea wakimbizi wengine endapo makambi yote mawili yatakuwa yamejaa.

Wakimbizi wote katika makambi yote mawili kwas asa wanapokea msaada sawa wa kibinadamu ambao unajumuisha mlo wa moto, usafiri, usajili, malazi, na huduma za ulinzi.

Timu zinazotoa huduma hizo pia zinaendesha ufuatiliaji ili kubaini watoto wasio na walezi au wazazi  na watu wenye mahitaji maalum walioko tayari katika vituo hivyo vya muda. “tunahakikisha msaada huu unaendelea kwa wakimbizi wote wapywa wanaowasili” limesema shirika hilo la wakimbizi.

UNHCR imewashukuru wote wanaohusika katika msaada huu wa kibinadamu unaoendelea ikiwemo KRI na wahudumu wengine wa misaada ya kibinadamu ambao wanafanya kazi saa 24 kuweza kuhakikisha wakimbizi wanapata malazi, huduma za msingi na ulinzi.

Pia shirika hilo limepeleka timu ya ziada ya wafanyakazi wa UNHCR kutoka ofisi yao ya Baghdad kwenda kkusaidia timu zao za Eibil na Dohuk kukidhi mahitaji ya wakimbizi wapya wanaowasili.