Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani

Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani. Wakulima wanawake ukanda wa Sahel.
©Artisan Productions / UNEP
Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani. Wakulima wanawake ukanda wa Sahel.

Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani

Tabianchi na mazingira

Nchi za Afrika katika ukanda wa Sahel zimechukua hatua Madhubuti kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa baiyonuai. Nchi hizo zinarejesha misitu na ardhi kwa kupanda miti katika eneo la urefu wa kilometa 8,000 kutoka magharibi hadi mashariki barani humo.

Mradi huo uliopatiwa jina la Ukuta Mkubwa wa Kijani ni mpango wa kipekee uliobuniwa kusaidia watu na mazingira kukabiliana na dharura ya tabianchi na mmomonyoko wa mifumo anuai muhimu na hatimaye kuzuia jangwa la Sahara kuenea zaidi katika nchi maskini zilizoko Sahel. 

Muungano wa Afrika, AU ulizindua mradi huo wa Ukuta Mkubwa wa Kijani mwaka 2007, mpango ambao  umetoka kuwa upandaji maji na kupanuka na kuwa mpango wa maendeleo vijijini. 

Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani.
©Artisan Productions / UNEP
Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani.

Hadi sasa maisha ya mamilioni ya watu yamebadilika kwani maeneo yaliyokuwa kame katika nchi 11 sasa yamekuwa ya kijani na kwa urahisi zaidi ekari takribani milioni 18 zilizokuwa zimemomonyoka sasa zimerejea katika hali ya kawaida. 

“Mpango huu wa kipekee tayari umeleta tofauti katika maisha ya watu wengi barani Afrika wakiwemo wale wanaoishi katika nchi zenye mizozo,” amesema Mirey Atalla, Mkuu wa kitengo cha mazingira kwa ajili ya tabianchi katika shirika la Umoja wa MAtaifa la mazingira duniani, UNEP akiongeza kuwa unaonesha manufaa makubwa ya urejeshaji wa udongo katika maeneo ambayo yako hatarini kuharibiwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Tayari mradi huo wa Ukuta Mkubwa wa Kijani umechaguliwa kuwa miongoni mwa miradi 10 muhimu ya urejeshaji wa maeneo ya ardhi katika Muongo wa UN wa urejeshaji wa bayonuai

Yatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2030, mradi huo utakuwe umeshaokoa ekari milioni 100 za ardhi, kufyonyza tani milioni 250 za hewa ya ukaa na kutoa fursa milioni 10 za ajira. 

Mradi ni fursa pia ya chakula na uhakika wa maji, eneo pia kwa ajili ya wanyama na mimea ya porini, na sababu tosha kwa wenyeji kusalia kwenye makazi yao yaliyoathiriwa kwa ukame na umaskini. 

Kurejesha mandhari kunatoa matumaini kwa siku zijazo katika eneo kame la Sahel.
©Artisan Productions / UNEP
Kurejesha mandhari kunatoa matumaini kwa siku zijazo katika eneo kame la Sahel.

Kuinua mipango ya wenyeji 

Licha ya kwamba jamii kuanzia Senegal, magharibi mwa Afrika hadi Ethiopia, mashariki mwa Afrika zinanufaika na mradi huo, kwa kiasi kikubwa mradi umejikita zaidi Burkina Faso na Niger. 

Mathalani manispaa ya Kollo nchini Niger ni moja ya manispaa nyingi ambako mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo, FAO na lile la mazingira, UNEP, mamlaka za serikali na wadau wengine wanasaidia jamii kurejesha misitu na udongo uliomomonyolewa. 

Msaada ukiwa  unatoka kwa wahisani kama vile Ufaransa na  Ujerumani, mradi unasaidia jamii huko Niger na nchi Jirani ya Burkina Faso kuanzisha miradi ya urejeshaji wa miti halikadhalika kujijengea uwezo ili hatimaye waanzishe miradi yao wenyewe. 

Mradi wa mfumo wa FAO wa kurejesha ardhi iliyomomonyoka, Christophe Besacier anasema wajasiriamali wa mazingira wanajengewa uwezo il ikuhakikisha utekelezaji wa uwekezaji endelevu kwenye sekta ya mazingira na wakati huo huo uwe na manufaa lukuki kwa jamii. 

“Nusu mwezi” wasaidia kuleta ukijani 

Mathalani manispaa ya Kollo, wakulima wameanzisha mbinu ya kijadi ya kunusuru ardhi iliyomomonyoka kwa kuchimba mashimo yenye umbo la mundu. 

Mashimo hayo wameyapatia jina ‘mashimo ya Zai” au ‘nusu mwezi,” ambapo mashimo hayo yana uwezo wa kuhifadhi maji ya mvua na kuyaelekeza kwenye mimea. 

Mbinu nyingine iliyothibitishwa inahusisha kuzungushia uzio kwenye ardhi ili kulinda miti na mioto mingine isiharibiwe na mifugo inayosaka malisho au wakata majani, na hivyo kupatia fursa miti kushamiri. Maeneo haya baadaye yanakuwa ni maeneo yenye mazingira bora kwa mazao au ufugaji nyuki. 

Djibo Dandakoye, Mkulima. Kufunga viwanja vya ardhi husaidia mimea na udongo kuzaliana na kuwa na rutuba nyingi.
©Artisan Productions / UNEP
Djibo Dandakoye, Mkulima. Kufunga viwanja vya ardhi husaidia mimea na udongo kuzaliana na kuwa na rutuba nyingi.

Djibo Dankakoye, mkulima huyu anasema, majani ya malisho ya ng’ombe kutoka kwenye eneo alilozungushia uzio huuzwa takribani dola senti 35 kwa furushi moja, na hicho ni chanzo endelevu cha mapato na kinatumiwa na familia zinazohudumia maeneo hayo, vijiji na manispaa. 

Zamani ardhi  hii ilikuwa kame na kavu,” anasema Dandokoye akiwa ameketi mbele ya mafurushi ya majani ya malisho ya ng’ombe. “Miti na majani unayoona sasa ni  matokeo ya kazi ngumu kutoka kwenye miti tuliyootesha na mbegu tulizopanda. Tulilipwa kwa kazi yetu na sasa tunavuna faida.” 

Wanawake wanachukua hatua 

Wanawake na wanaume nao wanafundishwa mbinu za kilimo cha misitu na mbinu nyingine za kujipatia kipato. 

Mradi umewezesha wanawake wa Kollo kupata ardhi ambako wanapanda miti aina ya Moringa, ambayo  majani yake yenye lishe na maganda ya mbegu yanaweza kuliwa kama mboga au kukaushwa na kusagishwa kuwa unga, inaweza kuwa mafuta au hata kutumika kuchujia maji. 

Ushirika umejenga duka dogo ambako wanawake wanaandaa na kuuza bidhaa zitokanazo na moringa. Bidhaa kama vile sabuni, kaukau na keki. 

Bi. Salamatou Souley, Meya wa Kollo. Mpango wa Great Green Wall ni kuwezesha jamii kupanga,  kutekeleza na kurejesha miradi ambayo inasaidia biashara ya ndani.
©Artisan Productions / UNEP
Bi. Salamatou Souley, Meya wa Kollo. Mpango wa Great Green Wall ni kuwezesha jamii kupanga, kutekeleza na kurejesha miradi ambayo inasaidia biashara ya ndani.

“Mti wa Moringa  una thamani kibiashara na unasaidia familia nyingi,” amesema Salamatou Souley, Meya wa Kollo. “Umebadilisha maisha ya wanaoupanda. Ni muhiu pia kuanzisha vikundi vya ushiriki kwa sababu kilimo cha Moringa kinaendana sawa kabisa na mradi wa urejeshaji wa ardhi.” 

Bi. Souley anasema kubadili mwelekeo wa kupotea kwa ardhi ya kilimo ilikuwa muhimu kwa ajili ya kuendeleza manispaa yake ya kijijini. 

“Motisha wangu ni kusongesha nafasi ya wanawake, kusaidia ujasiriamali wa wanawake na vijana na kuendeleza manispaa yangu, kwa njia moja au nyingine,” anatamatisha Souley. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2030 kuwa muongo wa kurejesha mfumo anuai duniani.