Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani:UNHCR

Nchini Niger kama maeneo mengine mengi ya Sahel, madhara ya mabadiliko ya tabianchi yamezidisha vipindi vya ukame na hivyo watu kuhama makazi yao na kusaka maeneo mengine huku wakitegemea zaidi  misaada
© FAO/IFAD/WFP/Luis Tato
Nchini Niger kama maeneo mengine mengi ya Sahel, madhara ya mabadiliko ya tabianchi yamezidisha vipindi vya ukame na hivyo watu kuhama makazi yao na kusaka maeneo mengine huku wakitegemea zaidi misaada

Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi UNHCR, limetahadharisha ongezeko la wakinbizi  huko Sahel na kutoa ombi la msaada wa haraka wa mahitaji ya kibinadamu kwa zaidi ya watu milioni 3.4 waliokimbia makazi yao na wenyeji wao kutokana na mafuriko makubwa yaliyozikumba nchi za Nigeria, Chad, Niger, Burkina Faso, Mali na Cameroon hivi karibuni. 

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinazidi kugharimu Maisha ya watu , katika Ukanda wa Sahel athari zinazidi kuongezeka zikichochewa na ukame, mafuriko, kupungua na kuzorota kwa mavuno ya mazao na kuzorota kwa jumla kwa huduma za umma na hivyo watu wengi kujikuta wakiyahama makazi yao.

Msemaji wa UNHCR Olga Sarrado akizungumza na waaandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi amesema katika nchi za Sahel ya Kati ambazo ni Niger, Mali na Burkina Faso mvua kubwa na mafuriko zimesababisha vifo vya mamia ya watu, maelfu kuyahama makazi yao, na kuharibu zaidi ya hekta milioni moja za ardhi ya kilimo.

Ameitaja nchi ya Nigeria kuwa inakabiliwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika muongo mmoja. “Mamia ya watu wamepoteza maisha, zaidi ya watu milioni 1.3 wamekimbia makazi yao, na zaidi ya watu milioni 2.8 wameathiriwa, kulingana na makadirio yaliyofanywa na Umoja wa Mataifa, huku mashamba na miundombinu ikisombwa.” Amesema Sarrado

UNHCR kwakushirikiana na mamlaka za mitaa, na washirika wengine wamekuwa wakiharakisha kutoa usaidizi wa kibinadamu na kufanya utambuzi wa maeneo ya kuwahifadhi manusura wa maafa hayo ya mafuriko.

Msemaji huyo wa UNHCR amesema “kwakushirikiana na washirika wetu tumekuwa tukitoa makazi na misaada muhimu kwa maelfu ya familia, ikiwa ni pamoja na maturubai 14,900 na seti 550 zenye vifaa vya msingi vya nyumbani. “

UNHCR inatoa ombi kwa wafadhili wote kutoa msaada wa haraka kwa wananchi wa Afrika Magharibi, Afrika ya Kati na Ukanda wa Sahel ili kuokoa maisha yao.