Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano, uongozi na kujitolea kunahitajika ili kufikia malengo ya maendeleo ya 2030: Mohammed

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Amina Mohammed ameelezea shangamoto zinazoukabili ukanda wa Sahel kwenye mkutano mjini Niamey Niger
UNECA/Daniel Getachew
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ameelezea shangamoto zinazoukabili ukanda wa Sahel kwenye mkutano mjini Niamey Niger

Mshikamano, uongozi na kujitolea kunahitajika ili kufikia malengo ya maendeleo ya 2030: Mohammed

Tabianchi na mazingira

Ingawa mizozo ya kimataifa inayoendelea inadhoofisha mafanikio ya maendeleo yanayopiganiwa kwa bidii, "sasa si wakati wa kukata tamaa", Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amewaambia mawaziri wa Afrika na watunga sera waliokutana mjini Niamey, Niger, hii leo.

Wakati huu ambapo bara la Afrika linakabiliana na athari za janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na vita nchini Ukraine, alisisitiza haja ya hatua kubwa zaidi kuchukuliwa ili kufikia mipango ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika ambayo imeahidi mustakabali jumuishi na endelevu kwa wote.

Tafuteni suluhu kutokea Afrika

"Katikati ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Ajenda 2063 tuko mbali na tunapohitaji kuwa," Bi. Mohammed alisema katika hotuba yake ya ufunguzi wa Kongamano la Tisa la Kikanda la Afrika la Maendeleo Endelevu.

"Lakini sasa sio wakati wa kukata tamaa. Kinyume chake, sasa ni wakati wa mshikamano, uongozi, na kujitolea kwa hatua tunazohitaji kuchukuliwa ili kutekeleza ajenda.

Alisema nchi zinaweza kubadili mkondo na kukabiliana na changamoto hiyo kupitia "suluhu zinazoongozwa na Afrika, zilizozaliwa katika ardhi ya Afrika", akibainisha kuwa Mkataba wa Biashara Huria wa Bara una uwezo wa kuwaondoa watu milioni 30 kutoka katika umaskini uliokithiri.

Mwanamke akinyunyizia maji mboga katika bustani ya soko iliyoanzishwa kwenye ardhi iliyoharibiwa zamani huko Ouallam, Niger. Bustani hiyo inashirikiwa na wakimbizi, watu waliokimbia makazi yao na wenyeji.
© UNHCR/Colin Delfosse
Mwanamke akinyunyizia maji mboga katika bustani ya soko iliyoanzishwa kwenye ardhi iliyoharibiwa zamani huko Ouallam, Niger. Bustani hiyo inashirikiwa na wakimbizi, watu waliokimbia makazi yao na wenyeji.

Mabadiliko ya nishati

Katika mkutano huo viongozi  wameidhinisha mpango kazi juu ya maendeleo endelevu ya viwanda na mseto wa kiuchumi.

"Lazima tuhakikishe kuwa uchumi unaoibukia wa kijani na kidijitali unahudumia vyema zaidi watu wa Afrika na mazingira asilia. Na ufunguo wa utekelezaji utakuwa ujumuishaji wa vijana wetu,” aliongeza.

Mabadiliko ya nishati barani Afrika ndio kiini cha juhudi hizi, alisema, akitoa mfano wa maendeleo yanayotia matumaini kama vile Usajili wa Mikopo ya Bonde la Kongo na mpango wa Ukuta mkubwa wa kijani huko ukanda wa Sahel.

Uwekezaji wenye kuleta suluhu

Bi Mohammed alisema viongozi wa dunia wanaokutana katika Mkutano wa SDG mwezi Septemba lazima waunge mkono na kuwekeza katika aina hizo za suluhu. Zaidi ya hayo, mkutano lazima utekeleze maeneo matatu muhimu, wakianzia na kuweka nguvu upya ahadi za kitaifa za SDG.

"Katika Mkutano huo, viongozi wa dunia lazima waweke wazi malengo ya kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa ifikapo 2027 na 2030. Na lazima wafanye hivyo kwa kuwekeza barani Afrika, uwekezaji katika uchumi wetu, na uwekezaji kwa watu wetu, hasa wanawake na vijana," alisema.

Kufadhili SDGs

Wanawake wakipanga foleni kupokea kadi za wanufaika wa misaada kwa ajili ya kununua unga ulioimarishwa ili kuzuia utapiamlo huko Kongoussi, Burkina Faso.
© WFP/Cheick Omar Bandaogo
Wanawake wakipanga foleni kupokea kadi za wanufaika wa misaada kwa ajili ya kununua unga ulioimarishwa ili kuzuia utapiamlo huko Kongoussi, Burkina Faso.

Maendeleo yanayoonekana kwenye ufadhili wa SDG lazima pia yawe matokeo mengine ya Mkutano wa kilele kwani "pengo la ufadhili kufikia SDGs na kutoa ustahimilivu wa mnepo wa mabadiliko ya tabianchi linaendelea kupanuka", alisema.

Bi. Mohammed aliripoti kwamba 43% ya mataifa ya Afrika yamo katika au karibu na dhiki ya madeni, hasa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao - hali aliyoelezea kuwa "haikubaliki".

"Katibu Mkuu ametoa wito kwa G20 kufungua kichocheo cha SDG cha angalau dola bilioni 500 kila mwaka kwa nchi zinazoendelea, hasa za Afrika," alikumbusha.

"Kwa upana zaidi, tunahitaji mageuzi ya kimfumo kwa usanifu wa kifedha wa kimataifa ambayo leo haifai kwa madhumuni na ambayo inabakia kuwa na mwelekeo wa muda mfupi, unaokabiliwa na migogoro, na kimsingi iliyoelekezwa kwa masilahi ya matajiri."

Ushirikiano

Mkutano huo lazima pia "uimarishe upya dhana ya ushirikiano wa kweli", aliendelea, akisisitiza haja ya kushirikiana na vijana, mashirika ya kiraia na umma wa kimataifa.

"Inamaanisha kupata matarajio makubwa na ya kuaminika zaidi ya SDG kutoka kwa biashara, sekta binafsi - huku tukipanua ushirikiano wa serikali za mitaa, baba zetu na mama zetu wa jadi, na kuwekeza katika sera za kisayansi," aliongeza.

Bi. Mohammed alisema katika miezi ijayo, UN itashirikiana na Serikali na washirika wengine kuendeleza maeneo hayo matatu, ikiwa ni pamoja na kupitia kazi ambayo tayari inafanywa na Waratibu Wakaazi, timu za nchi na taasisi za kikanda.

Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wanaongoza timu zinazohudumia zaidi ya nchi na wilaya 160 zinazounga mkono juhudi za Serikali za kufikia maendeleo endelevu.