Mchango wa sekta binafsi ni muhimu kwa SDGs:Espinosa

23 Oktoba 2018

Uwekezaji bora na ushirikishwaji wa wadau wote katika jamii ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu au SDGs. Kauli hiyo imetolewa leo mjini Geneva Uswis na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa alipozungumza na waandishi wa habari wa kimataifa kwenye makao makuu ya ofisi za Umoja wa Mataifa.

Bi. Espinosa amerejelea wito kwamba “tunahitaji ushiriki na uhusishwaji zaidi wa sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu “

Amesema uwekezaji wa sekta binafsi wa takribani dola trilioni 3.9 kwa mwaka unahitajika katika nchi zinazoendelea ili kuanzisha shughuli za kiuchumi ambazo zitasaidia kufikia matakwa ya malengo ya maendeleo endelevu ambayo ni kitovu cha ajenda ya 2030.

Espinosa amesema umoja wa Mataifa na dunia vinatambua kwamba kwa ajenda ya 2030 tunahitaji ajira, kwani ajira mpya milioni 600 zinapaswa kuundwa na kuongeza kuwa “Tuhahitahi uwekezaji zaidi na ulio bora, uwekezaji endelevu hususan katika maeneo kama ya teknolojia zitakazopunguza hewa ukaa, kwa mfano uwekezaji unaohitajika sana wa kuwa na uchumi unaojali mazingira, uwekezaji wa kuboresha ujumuishwaji na ushiriki wa wanawake na vijana, nadahani hatuwezi kufikiria uchumi jumuishi ambao utawaacha nusu ya watu wote nyuma.”

Amesema la msingi ni kuwawezesha wanawake na vijana na kwa kufanya hivyo kunatoa fursa ya kuchapuza maendeleo, kuongeza uzalishaji na kuchangia katika amani na usalama.

Bi. Espinosa amesema ukiangalia idadi kwanza utaona labda mambo ni mazuri katika idadi ya wabunge wanawake serikalini, lakini akiangalia vyema katika ngazi zingine za uongozi kama wakurugenzi watendaji wa sekta za makampuni binafsi idadi inashuka.

Rais huyo wa Baraza Kuu ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ecuador amekubuka jitihada alizokuwa akizifanya kuchagiza uimarishwaji wa sekta zote kama njia ya kutatua changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabia nchi, vita dhidi ya kifua kikuu na ukimwi, majanga ya asili, upokonyaji silaha na uhamiaji.

Amesisitiza kuwa “Njia pekee ya kushughulikia changamoto za kimataifa ni kupitia mtazamo wa mshikamano wa kimataifa na kuongeza kuwa hata kama tungeambiwa au kuona kila siku kwamba masuala ya kimataifa na maslahi ya kitaifa havichangamani, lakini nina imani kubwa kwamba inawezekana kutetea maslahi ya taifa na uhuru na wakati huohuo, tukashikamana katika hatua za pamoja na kubeba majukumu pamoja ya masuala muhimuvyo akasema “Hakuna njia nyingine yoyote ya kuweza kutatua changamoto zinazoighubika dunia na ambazo .”Hi zinaongezeka bila mshikamano wa kimataifa.”

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter