Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta za umma na binafsi zikishikamana zaweza kutokomeza umasikini na njaa:FAO

Mkulima katika shamba lake lililoshambuliwa na viwavi jeshi huko Namibia
FAO/Rachael Nandalenga
Mkulima katika shamba lake lililoshambuliwa na viwavi jeshi huko Namibia

Sekta za umma na binafsi zikishikamana zaweza kutokomeza umasikini na njaa:FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ufadhili wa sekta za umma pekee hautoshi kutimiza malengo ya maendeleo endelevu au SDG’s hivyo taasisi za maendeleo za kimataifa na za ufadhili lazima zishirikiane kujumuisha uwekezaji kutoka sekta binafsi.

Huo ni ujumbe uliotolewa leo kwenye kongamano la kimataifa mjini Marakech Morocco lililowaleta pamoja zaidi ya wawekezaji 200, wafanyabiashara, wawakilishi wa taasisi mbalimbali za maendeleo, watunga sera na maafisa wa serikali kutoka barani Afrika, Asia, Ulaya na nchi za Amerika.

Kongamano hilo lililoandaliwa na shirika la chakula na kilimo FAO kwa ushirikiano na Bank ya Ulaya ya ujenzi na maendeleo (EBRD) limefadhiliwa na Muungano wa Ulaya kwa lengo la kujadili fursa na changamoto katika kuwezesha uwekezaji wa sekta binafsi kwenye chakula na kilimo.

FAO inasema uwekezaji huo unahitaji uongozi imara na ushiriki wa wadau wote ikizingatiwa kwamba sekta ya chakula na kilimo inakabiliwa na mtihani mkubwa kote duniani, hususani katika masoko yanayochipukia.

Shirika hilo limeongeza kuwa, ili kuweza kuweka mazingira hayo mazuri ni muhimu kwa taasisi za fedha za kimataifa zikashirikiana na kuwekeza ipasavyo katika mfumo wa chakula na kilimo.

Vipaumbele ni pamoja na kuelewa vyma mahitaji ya sekta binafsi, uratibu mzuri wa kusaidia uwekezaji binafsi na kufanya kazi na serikali kuchagiza sera bora na mazingira mazuri ya biashara.

FAO inakadiria kwamba rasilimali za hadi za dola bilioni 265 zinahitajika kila mwaka ili kutokomeza umasikini na njaa ifikapo mwaka 2030. Hii ni takribani asilimia 0.3 ya makadirio ya wastani ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa hipindi hicho.