Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu ya kifo ni mkakati wa kuleta hofu, ni lazima ikomeshwe: Türk

Ishara ya maandamano ya kupinga adhabu ya kifo ikiinuliwa nje ya mahakama kuu mjini Washington DC nchini Marekani.
Unsplash/Maria Oswalt
Ishara ya maandamano ya kupinga adhabu ya kifo ikiinuliwa nje ya mahakama kuu mjini Washington DC nchini Marekani.

Hukumu ya kifo ni mkakati wa kuleta hofu, ni lazima ikomeshwe: Türk

Haki za binadamu

Kwa kutumia hukumu ya kifo dhidi ya waandamanaji, inaonekana mataifa yanapitisha mkakati unaokusudiwa kurejesha hofu miongoni mwa watu wanaoasi, ukandamizaji wa upinzani na kupiga marufuku matumizi halali ya uhuru, ameonya leo Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi.

Wakati wa mjadala kuhusu hukumu ya kifo katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, kamishna mkuu huyo Volker Türk, ameshutumu matumizi ya hukumu ya kifo, ambayo amesema "haikubaliki kwa binadamu yeyote. Hukumu ya kifo inapotumiwa dhidi ya watu ambao hata hawakufanya uhalifu wanaotuhumiwa, ni jambo lisilo halali”.

Bwana Türk ametanabaisha kuwa kuwepo kwa hukumu ya kifo katika nchi zinazoidumisha pamoja na tishio la matumizi yake inaweza kutumika kwa madhumuni yasiyofaa, kama vile kuleta hofu, kukandamiza upinzani na kunyima haki ya matumizi halali ya uhuru.

Katika miktadha kadhaa, hukumu ya kifo, katika utekelezwaji wake, pia ni ya kibaguzi, inayowahukumu kifo watu wasiojiweza katika jamii, ikiwa ni pamoja na makabila madogo, lugha za walio wachache, dini ndogo, na jamii ya LGBTQI-plus.

Mwanaharakati akiwa na ishara za kupinga adhabu ya kifo nje ya jengo la mahakama kuu ya Marekani mjini Washington.
© Unsplash/Maria Oswalt
Mwanaharakati akiwa na ishara za kupinga adhabu ya kifo nje ya jengo la mahakama kuu ya Marekani mjini Washington.

Hukumu ya kifo inatumika kama kizuizi

Katika hali nyingine, Bwana Türk amesema hukumu ya kifo imekuwa ikitumiwa na kuleta athari mbaya kwa wapinzani wa kisiasa au waandamanaji, haswa vijana. "Kwa kifupi, hukumu ya kifo ni, katika uzoefu wetu, ni mabaki ya kitabia ya zamani ambayo inapaswa kuachwa katika karne ya 2”.

Hata hivyo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ukweli unadhihirisha kwamba hukumu ya kifo ina athari ndogo au haina athari kabisa katika kuzuia au kupunguza uhalifu. Kwa kweli, tafiti nyingi zimegundua kwamba mataifa ambayo yameondoa hukumu ya kifo hayajaona mabadiliko yoyote katika viwango vyao vya mauaji na, katika hali zingine yamepungua.

Tafiti zingine zinaonyesha wazi kwamba jambo kuu ambalo watunga sera wanapaswa kuzingatia ni kutoepukika kwa adhabu, ambayo ni kizuizi chenye nguvu zaidi, badala ya kiwango chake cha ukali.

"Hata hivyo ninasikitishwa sana na ukweli kwamba hukumu ya kifo inaendelea kutumika, katika mazingira mbalimbali, kwa uhalifu ambao haukidhi kigezo cha uzito kilichowekwa na sheria za kimataifa," amesema kamishina huyo wa haki za binadamu.

Kuwe na mfumo utakaoheshimu haki

Katika suala hili kuhusu hukumu ya kifo, Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwe na mfumo wa kisheria wa kimataifa, ambao pia unahitaji kuheshimu kwa kina haki wakati wa kesi, ambalo ni muhimu sana katika kesi ya makosa yanayotolewa hukumu kama hio.

Mfumo ambao unakataza mateso au dhuluma, na unahakikisha haki za utetezi wa kutosha, kukata rufaa na kuomba msamaha au ubadilishaji wa hukumu ya kifo kuwa kifungo.

Hata hivyo Türk amesema pamoja na masharti haya yaliyo wazi, adhabu ya kifo bado inatumika vibaya kwa "makosa ya dawa za kulevya, ujasusi, uhalifu wa kiuchumi, kufuru na ukengeufu, mahusiano ya ushoga au uzinzi, na pia kwa upotovu na kwa utekelezaji halali wa uhuru wa raia. Katika nchi nyingi, bado tunashuhudia ushinikizaji wa hukumu ya kifo, ambao hauendani na viwango vya haki vya kesi."

Chini ya masharti haya, Umoja wa Mataifa umepinga hukumu ya kifo kwa miaka mingi. "Katika muktadha wa hukumu ya kifo, ina maana tu kwamba watu wasio na hatia wameuawa," amesema Türk, akihimiza mataifa ambayo hayajakomesha matumizi ya hukumu ya kifo kusitisha sasa na kufanya kazi kuelekea ukomeshaji kabisa wa hukumu hiyo.

Tukio la hali ya juu kuhusu hukumu ya kifo.
UN Photo
Tukio la hali ya juu kuhusu hukumu ya kifo.

Mataifa 26 ya Afrika yamefuta kabisa hukumu ya kifo

Kwa upande wake, chombo cha Muungano wa Afrika AU kimetaja baadhi ya matifa yaliyoamua kuchukua hatua kutokana na mienendo ya sasa  ya sababu ya ukomeshaji wa hukumu ya kifo katika bara la Afrika.

Kulingana na Rais wa kikosi kazi cha adhabu ya kifo cha tume ya Afrika ya Haki za binadamu na Watu (ACHPR), mwaka wa 2022 ulimalizika kwa nuru ambapo Jamhuri ya Zambia ilipitisha sheria inayoondoa kabisa hukumu ya kifo kwa makosa yote kwa wote.

Mageuzi haya makubwa yanafuatia mipango kama hiyo iliyotekelezwa hapo awali na nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na Ecuatorial Guinea.

"Zaidi ya hayo, takwimu zilizopo zinaelezea mwelekeo wa ukomeshaji hukumu ya kifo ambao unaendelea kwa uwazi katika bara hili. Hadi sasa mataifa 26 yamechagua kukomesha kabisa hukumu ya kifo huku wengine wasiopungua 14 wakiomba kusitishwa kabisa kwa utekelezaji wa adhabu hii ya kifo." amesisitiza Idrissa Sow.

Kwa upana zaidi, ACHPR inasalia kushawishika juu ya haja ya kuendeleza hatua za ushirikiano na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa ili kusonga mbele kwa uthabiti kuelekea kufikiwa kwa lengo kuu ambalo linasalia kuwa ni kukomeshwa kwa adhabu ya kifo kwa wote barani humo kupitia mkabala wa kimaendeleo ambao unatilia mkazo zaidi haki ya urejeshaji inayohusika na utekelezaji kamili kwa sharti la kulinda haki ya kuishi.

Kwa mantiki hiyo inazihimiza mara kwa mara Mataifa haya kuweka ukomo wa matumizi ya adhabu ya kifo kwa makosa makubwa zaidi tu na kuzingatia uanzishwaji wa kusitisha unyongaji huku ikisubiri kufikiria kukomesha kabisa adhabu hiyo ya kifo.

Hata hivyo, pamoja na jitihada zote zilizofanywa, ACHPR inatambua kwamba hukumu ya kifo inaendelea kutamkwa katika bara la Afrika, "wakati mwingine kwa mamlaka ya kipekee, na hatari za wazi zakutotimizwa haki kutokana na udhaifu wa mifumo ya mahakama katika nchi nyingi ".