Hukumu ya kifo kwa madai ya kukashifu dini Pakistan ni ukiukwaji wa haki: Wataalam UN

27 Disemba 2019

Watalaam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamelaani vikali hukumu ya kifo aliyopewa mhadhiri wa chuo kikuu cha Bahauddin Zakariya nchini Pakistan kwa madai ya kukashifu dini.

Wataalam hao wamesema mhadhiri huyo Junaid Hafeez mwenye umri wa miaka 33 alitiwa mbaroni 13 Machi mwaka 2013 kwa shutuma za kutumia maneno ya kashifa dhidi ya dini wakati akifundisha darasani na kwenye mtandao wake wa Facebook, na kufunguliwa mashitaka chini ya sheria ya kashifa dhidi ya dini nchini humo.

Na tangu mwaka 2014 kesi yake ilipoanza kusikilizwa amekuwa kifungoni akiwa ametengwa na wafungwa wengine hali ambayo imemuathiri vibaya afya ya mwili na akili .

Wataalam hao huru wamesema na baada ya miaka mitano ya kuwepo kifunguni Desemba 21 mwaka 2019 Hafeez akihukumiwa kifo na mahakama ya wilaya na mahakama ya kanda ya Multan nchini Pakistan.

Kwa mujibu wa wataalam hao hukumu hiyo si haki na ni ukiukwaji wa haki za binadamu huku wakisisitiza kwamba “inaonekana kuna mazingira ya hofu miongoni mwa wafanyakazio wa mahakama waliokuwa wakiendesha kesi hii hali ambayo inaelezea kwa nini takriban majaji sana walihalimshwa wakati wa kusikiliza kesi hii iliyochukua muda mrefu.”

Wataaalam hao wamesema hukumu hiyo imetolewa licha ya uamuazi wa mahakama kuu dhidi ya kesi ya mwaka jana ya Asia Bibi iliyohusu kukashifu dini pian a ombi la haraka la wataalam huru wa Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Pakistan wakielezea msingi wa uhalali wa kisheria  kuhusu kesi hiyo.

“Uamuzi wa mahakama kuu kuhusu hukumu ya kesi ya Asia Bibi ulipaswa kutumika kama mfano kwa mahakama za chini kufuta kesi yoyote ya madai ya kukashifu dini ambayo haijathibitishwa kwa kina.”

Wameongeza kuwa kwa kutolewa hukumu ya kukutwa na hatia katika kesi hii dhidi ya Bwana Hafeez ni ukiukwaji wa haki na tunalaani vikali hukumu ya kifo dhidi yake. “Tunazitaka mahakama za juu za serikali ya Pakistan kusikiliza rufaa ya Hafeez, kutengua hukumu ya kifo na kumuachia huru”

Kwa mujibu wa wataalam hao katika sheria za kimataifa hukumu ya kifo inaruhusiwa tu katika mazingira maalum na inahitaji ushahidi wa haki na wa kutosheleza wa mauaji ya kimataifa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter