Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari ya vita kwa watoto Ukraine haijawahi kushuhudiwa tangu vita ya pili ya dunia:UNICEF 

Msichana wa miaka 9 akisimama kwenye eneo la kuegeza magari Kharkiv ambako ametafuta hifadhi na wazazi wakati wa mzozo Ukraine.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Msichana wa miaka 9 akisimama kwenye eneo la kuegeza magari Kharkiv ambako ametafuta hifadhi na wazazi wakati wa mzozo Ukraine.

Athari ya vita kwa watoto Ukraine haijawahi kushuhudiwa tangu vita ya pili ya dunia:UNICEF 

Amani na Usalama

Takriban siku 100 za vita nchini Ukraine zikikaribia, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema athari kubwa za vita hivyo kwa watoto hazijawahi kushuhudiwa tangu vita ya pili ya dunia. 

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva inasema watoto milioni tatu ndani ya Ukraine na zaidi ya watoto milioni 2.2 katika nchi zinazohifadhi wakimbizi sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu.  

Takriban watoto wawili kati ya watatu wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano. 

Kulingana na ripoti zilizothibitishwa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, kwa wastani zaidi ya watoto wawili huuawa na zaidi ya wanne kujeruhiwa kila siku nchini Ukraine hasa katika mashambulizi ya kutumia silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi.  

Miundombinu ya kiraia ambayo watoto hutegemea inaendelea kuharibiwa au kubomolewa na hadi sasa inajumuisha angalau vituo vya afya 256 na moja kati ya shule sita zinazosaidiwa na UNICEF katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo. Mamia ya shule nyingine kote nchini pia zimeharibiwa. Hali kwa watoto Mashariki na kusini mwa Ukraine ambako mapigano yameongezeka inazidi kuwa mbaya. 

Siku ya kuwalinda watoto Ukraine 

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell leo "Tarehe 1 Juni ni siku ya kimataifa ya ulinzi wa watoto nchini Ukraine na kote katika kanda hiyo. Badala ya kusherehekea hafla hiyo, tunaikaribia sana Juni 3  siku ya 100 ya vita ambavyo vimesambaratisha maisha ya mamilioni ya watoto. Bila ya usitishaji wa vita wa dharura na majadiliano ya amani, watoto wataendelea kuteseka na kuanguka kutokana na vita hivyo kutaathiri watoto walio katika mazingira magumu ulimwenguni kote." 

UNICEF pia inaonya kwamba vita hivyo vimesababisha mgogoro mkubwa wa ulinzi wa watoto.  

Watoto wanaokimbia machafuko wako katika hatari kubwa ya kutengana na familia zao, ukatili, unyanyasaji, unyanyasaji wa kingono, na usafirishaji haramu wa binadamu.  

Shirika hilo linasema wengi wamekabiliwa na matukio ya kutisha sana. “watoto hawa wanahitaji kwa dharura usalama, uthabiti, huduma za ulinzi wa watoto, na usaidizi wa kisaikolojia hasa wale ambao hawajaandamana au wametenganishwa na familia zao. Zaidi ya yote, wanahitaji amani.” Ameongeza Bi. Russel. 

Wakati huohuo, ameongeza vita na watu wengi kuhama makazi yao ni hatari sana kwa maisha na fursa za kiuchumi, na hivyo kuacha familia nyingi bila mapato ya kutosha kukidhi mahitaji ya msingi na kushindwa kutoa msaada wa kutosha kwa watoto wao. 

Mvulana wa miaka 10 akitembea mbele ya jengo lao katikati mwa Chernihiv, Ukraine lilioharibiwa na shambulizi la anga.
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Mvulana wa miaka 10 akitembea mbele ya jengo lao katikati mwa Chernihiv, Ukraine lilioharibiwa na shambulizi la anga.

Usitishaji uhasama ndio suluhu pekee 

UNICEF inaendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja nchini Ukraine na kuwalinda watoto wote dhidi ya madhara ya vita hivyo. 

Hii ni pamoja na kukomesha matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi na mashambulizi kwenye miundombinu ya kiraia.  

UNICEF inaomba fursa ya kufikisha kikamilifu  msaada wa  kibinadamu na kwa usalama na haraka kwa watoto  wote wanaohitaji msaada huo popote walipo. 

UNICEF na washirika wake wako nchini Ukraine na nchi jirani, wakifanya kazi ya kuwapa watoto na familia zao msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa watoto, maji na usafi wa mazingira, afya, lishe na huduma za elimu. 

Nchini Ukraine, UNICEF na washirika wamesambaza vifaa vya afya na matibabu vya kuokoa maisha kwa karibu watu milioni 2.1 katika maeneo yaliyoathiriwa na vita kuwezesha upatikanaji wa maji salama kwa zaidi ya watu milioni 2.1 wanaoishi katika maeneo ambayo mitandao imeharibiwa au kusambaratishwa, pia wamewafikia zaidi ya watoto na walezi 610,000 kwa msaada wa afya ya akili na kisaikolojia na kutoa vifaa vya kujifunzia kwa karibu watoto 290,000.  

Takriban familia 300,000 zilizo katika mazingira magumu zimejiandikisha kwa ajili ya mpango wa usaidizi wa kibinadamu wa kifedha wa idara ya Sera ya kijamii wa UNICEF.


Msaada kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi 

Katika nchi zinazohifadhi wakimbizi, UNICEF inasaidia mifumo ya kitaifa, manispaa na mitaa ambayo inatoa huduma muhimu na ulinzi, haswa kwa watoto walio hatarini zaidi.  

Hii ni pamoja na mafunzo ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa walinzi wa mpakani, kupanua wigo wa fursa za kujifunza na kuwajumuisha watoto wakimbizi shuleni, ununuzi wa chanjo na vifaa vya matibabu na kuanzisha vituo vya kucheza na kujifunzia ambavyo vinawapa watoto wadogo hisia zinazohitajika sana za hali ya kawaida na muhula wa shule.  

Maeneo 25 ya UNICEF-UNHCR Blue Dots ambayo ni maeneo salama hutoa usaidizi na huduma kwa familia zinazosafiri, yameanzishwa kando ya njia kuu za usafiri huko Moldova, Romania, Poland, Italia, Bulgaria na Slovakia.  

Nchini Moldova, zaidi ya wakimbizi 52,000, wengi wao wakiwa katika kaya zinazoongozwa na wanawake, wamefikiwa kupitia mpango wa usaidizi wa fedha wa malengo mbalimbali wa UNICEF na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. 

UNICEF imetoa ombi la  dola milioni $624.2 kwa ajili ya fedha za kusaidia jhatua zake za kibinadamu ndani ya Ukraine na ombi la dola milioni $324.7 kwa hatua zake za msaada katika nchi zinazohifadhi wakimbizi.