Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Tanzania kwa kuendelea kuwa kimbilio la waliofurushwa makwao- Grandi

Akiwa ziarani nchini Tanzania, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi (wa pili kushoto) alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mji mkuu, Dodoma.
Ikulu Tanzania
Akiwa ziarani nchini Tanzania, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi (wa pili kushoto) alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mji mkuu, Dodoma.

Heko Tanzania kwa kuendelea kuwa kimbilio la waliofurushwa makwao- Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amekuwa na mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili maendeleo katika kuweka mazingira mazuri kwa wakimbizi wa Burundi walioko nchini humo kurejea nyumbani.

Tweet URL

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema mazungumzo hayo yamefanyika Dodoma, mji mkuu wa Tanzania ambako Bwana Grandi alifika baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Burundi.

Kamishna Mkuu Grandi amepongeza utamaduni wa muda mrefu wa Tanzania wa kukaribisha wakimbkizi, sambamba na juhudi za taifa hilo za kuendelea kukidhi mahitaji ya wale wanaokimbia ghasia makwao.

Takribani wakimbizi 248,000 na wasaka hifadhi wengi wao kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wanaishi nchini Tanzania, taifa ambalo linaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kutoka Burundi.

Timu zetu zitaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya Burundi na Tanzania, wadau na wahisani wakiwemo wale wa maendeleo ili kulinda na kusaka majawabu ya wale waliokimbia makwao,” amesema Bwanda Grandi.

Katika muktadha huo, UNHCR imekaribisha tangazo la hivi karibuni la Muungano wa Ulaya, EU, la kutoa dola 42,700 katika kipindi cha miaka ijayo ili kusaidia changamoto nchini Burundi.

Fedha hizo, kwa mujibu wa UNHCR, zitatumika kuhakikisha wakimbizi wa Burundi kwenye ukanda huo wa Maziwa Makuu pamoja na wale waliorejea nyumbani wanapata msaada wanaohitaji ili waishi kwa utu na usalama.

Msaada huo ni pamoja na ulinzi, kujengewa mnepo wa kujikimu kimaisha, msaada wa sheria, na kuzuia na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia, sambamba na elimu ya kuwawezesha kujua kusoma na kuandika na kilimo.