Msaada zaidi kwa Tanzania wahitajika ili ihudumie vyema wakimbizi- Grandi

8 Februari 2019

Kamishna Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa ,UNHCR, Filippo Grandi amehitimisha ziara yake ya siku nne nchini Tanzania akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwekeza zaidi mikoa ya kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo ambayo ni nyumbani kwa wakimbizi 330,000. 

Ziara hiyo ya siku nne ilimfikisha Bwana Grandi kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma nchini Tanzania ambako alishuhudia jinsi wakimbizi walivyo na matumaini licha ya kuishi ugenini.

Akiwa kambini alikutana na mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Selemani Boaz ambaye ni mchuuzi kambini humo na akimweleza kuwa soko hilo linasaidia utangamano na wenyeji na pia wakimbizi wanapata vyakula tofauti na vile vya msaada.

UNHCR/Georgina Goodwin
Soko la pamoja ambako wakimbizi kutoka Burundi na DR Congo wanaweza kukutana na wenyeji watanzania walio jirani na kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma nchini Tanzania.

Kisha alijerejea Dar es salaam ambako alizungumza na waandishi wa habari akipongeza jinsi taifa hilo la Afrika Mashariki lilivyoendelea kuwa pepo ya wale wanaokimbia ghasia nchini mwao, akisema,  “ni muhimu kwamba hakuna tu anayelazimishwa kurejea nyumbani na zoezi la kurejea ni la hiari. Tunaomba usaidizi zaidi wa kimataifa ili kuhakikisha wakimbizi wanaorejea nyumbani kwa hiari wanaweza kutangamana na jamii zao na pia kusaidia kuwezesha ufuatiliaji kwa kuwa hivi sasa fedha hazitoshelezi.”’

Naye Naibu Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania Zephania Amuiri amezungumzia huduma kambini akigusia huduma ya afya akisema kwa magonjwa kama vile saratani na afya ya akili huwa wanaomba kuhamishia wagonjwa kwenye hospitali kama vile Bugando mkoani Mwanza na Muhimbili jijini Dar es salaam.

Hata hivyo amesema wakati mwingine wanaomba madaktari mabingwa wafike kambini ili kutoa huduma kwa wakimbizi wengi zaidi.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter