Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR awataka wahisani kuisaidia Tanzania wakati ikiendelea kukirimu wakimbizi

Mkimbizi kutoka Burundi anayeishi kwenye kambi ya Nduta mkoani Kigoma nchini Tanzania .
UNHCR/Benjamin Loyseau
Mkimbizi kutoka Burundi anayeishi kwenye kambi ya Nduta mkoani Kigoma nchini Tanzania .

Mkuu wa UNHCR awataka wahisani kuisaidia Tanzania wakati ikiendelea kukirimu wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR amewahimiza wahisani kuunga mkono zaidi suluhu za suala la wakimbizi na kusifu maendeleo yaliyopigwa katika ulinzi wa wakimbizi nchini Tanzania.

Filippo Grandi, ameyasema hayo akihitimisha ziara yake leo nchini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema miongoni mwa suluhu hizo ni pamoja na hatua endelevu ya wakimbizi kurudi nyumbani kwa hiari.

Katika ziara yake ya siku tatu, Grandi amekutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na kujadili umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya kurejea kwa wakimbizi wa Burundi, huku akihakikisha wakimbizi wote nchini Tanzania wanalindwa na kusaidiwa.

Wakimbizi wanaohifadhiwa Tanzania

Wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kutoka Tanzania wakiwa kwenye kituo cha mpito cha Mabanda katika jimbo la Makamba nchini Burundi. (24 Aprili 2018)
OCHA/Christian Cricboom
Wakimbizi wa Burundi wanaorejea nchini mwao kutoka Tanzania wakiwa kwenye kituo cha mpito cha Mabanda katika jimbo la Makamba nchini Burundi. (24 Aprili 2018)

Kwa sasa Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi 248,000, hasa kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na wengi wao wanaishi katika kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu katika mkoa wa Kigoma nchini humo. 

Tangu Septemba 2017, takriban wakimbizi 142,000 wa Burundi wamerejea nyumbani Burundi kwa hiari.

Grandi ameipongeza Tanzania na wananchi wake kwa historia yao ya muda mrefu ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi, pamoja na juhudi za kuendeleza ulinzi na suluhisho kwa wakimbizi nchini humo, kwa kuzingatia mkataba wa kimataifa wa wakimbizi.

"Kwa kweli nimetiwa moyo na juhudi za serikali za kuimarisha ulinzi wa wakimbizi, na kusimama pamoja nao. Ahadi ya UNHCR ya kuunga mkono Tanzania na kulinda haki za wakimbizi wanaohifadhiwa hapa bado ni thabiti."

Katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, kaskazini magharibi mwa nchi, Grandi amekutana na wakimbizi wa Burundi na Congo, washirika na mamlaka za za eneo hilo. 

Pia ametembelea kituo cha ufundi stadi katika kambi hiyo ambapo wakimbizi na Watanzania kutoka vijiji vya jirani walikuwa wakijifunza ujuzi wa vitendo kama ushonaji nguo na ulimaji wa bustani ya mboga mboga bega kwa bega. 

Grandi alitangamana na jamii zinazohusika katika mradi wa jamii wa uzalishaji wa mkaa usiochafua mazingira briketi, ambao unalenga kupunguza utegemezi wa kuni na kuzuia uharibifu wa mazingira.

Mawio kambini Nduta mkoani Kigoma nchini Tanzania ambako ni makazi ay wakimbizi kutoka Burundi.
UNHCR/Sebastian Rich
Mawio kambini Nduta mkoani Kigoma nchini Tanzania ambako ni makazi ay wakimbizi kutoka Burundi.

Heko Tanzania kutoa vyeti vya kuzaliwa

Kamishina huyo wa wakimbizi Amepongeza juhudi za hivi karibuni za Serikali ya Tanzania za kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wakimbizi, akibainisha kuwa hatua hiyo itawapa ulinzi muhimu wa kisheria na kupunguza hatari ya kutokuwa na utaifa, huku pia ikitoa aina ya utambulisho wanaporejea katika nchi yao ya asili.

Pia ameshuhudia jinsi upungufu wa ufadhili unavyoathiri moja kwa moja juhudi za kibinadamu mashinani. 

Kufikia Agosti 2022, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 27 pekee ya fedha zinazohitajika nchini Tanzania kwa mwaka huu.

"Hali ya Burundi bado haijafadhiliwa kwa kiasi kikubwa. Natoa wito kwa wafadhili, wakiwemo washirika wa maendeleo, kutoa fedha na uwekezaji nchini Tanzania na kuongeza utoaji wa huduma za msingi. Ukosefu wa ufadhili unaweza kuhatarisha kurudisha nyuma juhudi zilizopatikana kwa bidii. “

Pia ametoa wito wa kuimarishwa kwa usaidizi nchini Burundi ili kusaidia kukabiliana na vikwazo vinavyozuia wakimbizi kurudi nyumbani.

Grandi amesisitiza kuwa "Tanzania kwa zaidi ya miongo minne imekuwa ikihifadhi kwa ukarimu idadi kubwa ya wakimbizi, na hatupaswi kuwaangusha. Tutaendelea kufanya kazi na serikali na washirika kuboresha ustawi na maisha ya wakimbizi na jamii zinazowapokea nchini Tanzania, na kusaidia kurejea kwa hiari kwa wakimbizi nchini Burundi.”

Ziara ya Grandi Tanzania inafuatia mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyoitishwa na serikali ya Tanzania na UNHCR mwezi Machi 2022 ili kukubaliana kuhusu hatua za kuimarisha ulinzi na ufumbuzi wa chngamoto za wakimbizi.