Tumeomba mazungumzo na UN wasaidie hali Burundi ili kuandaa Tanzania  kuwarejesha wakimbizi - Rais Samia 

26 Oktoba 2021

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika mashariki ambazo zimekuwa kimbilio la wakimbizi kwa miaka mingi. Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan alipozungumza na Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa alipokuwa hapa New York, Marekani anasema ni takribani miaka 50 kwa nyakati tofauti nchi yake imekuwa ikipokea wakimbizi na kwa sasa ameomba mazungumzo na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia wakimbizi UNHCR kusaidia katika nchi wanakotoka wakimbizi ili waweze kurejea akitolea mfano Burundi.

Rais Samia anaanza kwa kueleza hali ya wakimbizi ilivyo hivi sasa nchini Tanzania akisema, "tuna wakimbizi takribani 347,600 na kitu hivi kutoka Burundi.Lakini tua wakimbizi wengine kama 200,000 na hivi kutoka DRC na wengine kama 368 wa mataifa mbalimbali. Hawa wa mataifa mbalimbali hawatupi shida kwa sababu wapo tunajua wapo. Lakini wale ambao wako kwenye makambi pale Kigoma, tuna makambi matatu ya wakimbizi. mwaka juzi tulifanya mazungumzo na tukakubaliana kuwarudisha, sisi na lile shirika linalohudumia wakimbizi, UNHCR, tukakubaliana kuwarudisha nyumbani na tukaanza kazi ya kuwarudisha nyumbani wale wa Burundi. "

Kuhusu wakimbizi wa DRC Rais Samia amesema "Hatuwezi kuwarudisha kwa sababu bado hakujatengamaa vizuri. Lakini Burundi tunashukuru sana Rais Evariste Ndayishimiye ameifanya Burundi imetulia, usalama uko wa kutosha na tukaanza kurudisha wakimbizi. Kinachotokea ni nini; wakifika Burundi hawana ardhi hawana nyumba, hawana pa kufikia. Na mapokezi pia wanaonekana kwamba mlienda wapi kwa nini mmerudi. Kwa hivyo wanajikuta hawako mahali pazuri, hawapokewi wanatafuta njia za kurudi tena nyumbani." 

Na kwa msingi huo, Rais Samia anaongeza akisema, "tumeomba mazungumzo na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbiziUNHCR lakini pia mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kwamba waende wasaidie kule Burundi, hali itengamae kule Burundi kuwe na mipango yote ya kupokea wakimbizi na kuwafanya waweze kuishi ndani ya nchi yao. Tukiweza kufanya hivyo, wataweza kurejea nyumbani kwao. Lakini bila kufanya hivyo wanarejea Tanzania. Na wanaporudi hatuwezi kuwafukuza kwa sababu tumesaini mikataba ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa kwamba tutapokea na tutawatunza wakimbizi."

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter