Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wavamia vituo vya MONUSCO Kivu Kaskazini na kupora mali

Mlinda amani wa MONUSCO akiwa kwenye lindo katika kituo cha ujumbe huo mjini Walikale jimboni Kivu Kaskazini
MONUSCO
Mlinda amani wa MONUSCO akiwa kwenye lindo katika kituo cha ujumbe huo mjini Walikale jimboni Kivu Kaskazini

Raia wavamia vituo vya MONUSCO Kivu Kaskazini na kupora mali

Amani na Usalama

Leo asubuhi kwa saa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waandamanaji wamevamia vituo vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCI kwenye mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini ambako wamepora mali, wamerusha mawe na kuchoma moto matairi ya magari.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo, amesema “waandamanaji walilenga vituo vya MONUSCO huko Goma, wakaweka vizuizi barabarani. Walinda amani walilazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za maonyo kwa ajili ya kulinda wafanyakazi na hospitali ya Umoja wa Mataifa na miundombinu mingine muhimu.”

Bwana Haq amesema kulikuweko pia na tukio kama hilo kwenye kituo cha MONUSCO huko Nyamilima, kilometa 38 kaskazini-mashariki mwa mji wa Rutshuru.

“Walinda amani kadhaa wamepata majeraha kidogo,” amesema Bwana Haq akiongeza kuwa huko Kitchanga, kilometa 28 kaskazini-mashariki mwa mji wa Masisi nako pia kulikuweko na maandamano lakini ya amani.

Taarifa ya MONUSCO ilotolewa leo kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa imelaani matukio hayo ikirejelea suala kwamba, “maeneo ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuvamiwa kwa mujibu wa makubaliano kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya DRC kuhusu hadhi ya majeshi, SOFA.”

Wakati huo huo, MONUSCO imeanza kutumia itifaki za nyongeza za usalama na sambamba na mipango ya kwenda na mazingira ili kuhakikisha utekelezaji wa mamlaka yake ya usalama na ulinzi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.