Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 100,000 wametawanywa na makumi kuuawa wiki iliyopita DRC:UN

Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma DRC, (Kutoka Maktaba)
© MONUSCO/Sylvain Liechti
Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma DRC, (Kutoka Maktaba)

Watu 100,000 wametawanywa na makumi kuuawa wiki iliyopita DRC:UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema raia zaidi ya 100,000 wametawanywa na machafuko yanayoendelea Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC huku wengine kwa makumi wakiuawa kwa kipindi cha wiki moja iliyopita pekee.

Akizungumza na waandishi a habari mjini New York Marekani hii leo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dijarric amesema “kwa mujibu wa taarifa tulizopewa na washirika wetu wa kibinadamu, zaidi ya watu 50,000 waliokimbia makazi yao kutoka Rutshuru wamepata usalama huko Kibirizi, wakati watu wengine 55,000 kutoka Masisi wamekimbilia vijiji jirani na Goma na kuelekea Minova katika jimbo la Kivu Kusini.”

Ameongeza kuwa walinda amani wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO wameripoti kwamba wamewahifadhi watoto 95 katika kituo chao cha Sake, ambacho kinajumuisha watoto  wengine 50 kutoka kituo cha watoto yatima. Na hii imetokea kufuatia mapigano ya mwishoni mwa wiki katika eneo hili kati ya vikosi vya ulinzi vya jeshi la Congo na kundi la waasi la M23. Raia wanne walifariki dunia wakati wa mapigano hayo na takriban wengine watano kujeruhiwa. Askari wa kulinda amani walitoa msaada wa matibabu kwa waliojeruhiwa kwenye kituo chao na baadaye kuwahamisha hadi Goma. Watoto hao pia walihamishiwa katika kituo cha watoto huko Goma.”

Familia iliyotengana wakikimbia ghasia mashariki mwa DRC imeunganishwa tena mjini Goma. (Maktaba))
© UNICEF/Jospin Benekire
Familia iliyotengana wakikimbia ghasia mashariki mwa DRC imeunganishwa tena mjini Goma. (Maktaba))

Tangu mwanzo wa Machi watu 97 wameuawa

Taarifa hiyo ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa MONUSCO imeripoti kwamba “tangu mwanzoni mwa mwezi Machi, kundi la waasi la ADF limeripotiwa kuwaua takriban raia 97 katika eneo la Beni, kwnye jimbo la Kivu Kaskazini.”

Pia amesema kutokana na operesheni za pamoja zinazoendelea kati ya vikosi vya ulinzi vya Uganda na Congo, walinda amani wa Umoja wa Mataifa hawawezi kufikia eneo la kusini mwa Beni, ambako watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa ADF walifanya mashambulizi haya.

“Sisi pamoja na washirika wetu wa kibinadamu tunatoa msaada wa kiafya, elimu, chakula, maji na usafi wa mazingira miongoni mwa huduma zingine zinazohitajika kwa maelfu ya watu katika mji wa Beni na maeneo jirani. Pia tunashughulikia kuongeza hatua zetu za usaidizi.”

Katika jimbo la Kivu Kaskazini, katika mwaka uliopita, elimu ya zaidi ya watoto 600,000 imeathiriwa na vurugu zinazoendelea.

Amekumbusha kwamba katika mwaka uliopita, ghasia mpya katika eneo hilo zimesababisha zaidi ya wanaume,wanawake na watoto 800, 000, kuyahama makazi yao.

Na hivi sasa nchini DRC, zaidi ya watu milioni 6 ni wakimbizi wa ndani.