Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ni haki ya msingi ya binadamu kila mtu anastahili kuipata: Guterres

Wasichana wadogo wakitembea kuelekea nyumbani kutoka shuleni huko Sao Tome, Sao Tomé e Principe.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Wasichana wadogo wakitembea kuelekea nyumbani kutoka shuleni huko Sao Tome, Sao Tomé e Principe.

Elimu ni haki ya msingi ya binadamu kila mtu anastahili kuipata: Guterres

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya elimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba elimu ni haki ya msingi ya binadamu na hivyo kila mtu anastahili kuipata. 

Kupitia ujumbe wake wa siku hii inayoadhimishwa kila mwaka Januari 24 Antonio Guterres amesema “Ni msingi wa jamii, uchumi, na uwezo wa kila mtu. Lakini bila uwekezaji wa kutosha, uwezo huu utaishia kwenye mzabibu. 

Imekuwa jambo la kushangaza kwangu kwamba elimu imekuwa ikipewa kipaumbele cha chini sana katika sera nyingi za serikali na katika vyombo vya ushirikiano wa kimataifa.” 

Kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya elimu mwaka huu inakumbusha “Kuwekeza katika watu na kutoa kipaumbele katika elimu.” 

Uwekezaji ni muhimu kutimiza SDG-4 

Bwana Guterres ameendelea kusema kwamba uwekezaji ni muhimu katika kufikia lengo la 4 la maendeleo endelevu linalohusu elimu kwa wote. 

Amekumbusha kwamba mkutano wa mwaka jana wa mabadiliko ya elimu uliuleta ulimwengu pamoja ili kufikiria upya mifumo ya elimu ili kila mwanafunzi apate maarifa na ujuzi unaohitajika kuweza kufaulu. 

Zaidi ya nchi 130 zilijitolea kuhakikisha kuwa elimu bora kwa wote inakuwa nguzo kuu ya sera na uwekezaji wa umma. 

Ujumbe wake umefafanua kuwa “Wito wa kuchukua hatua kuhusu uwekezaji wa kielimu na kuanzishwa kwa kituo cha kimataifa cha ufadhili wa elimu vilileta msukumo mpya wa ufadhili wa ndani na kimataifa.” 

Na mkutano huo ulizindua mipango mbalimbali ya kimataifa ya kuhamasisha usaidizi wa elimu katika mazingira ya migogoro, elimu ya wasichana, mafunzo ya msingi, kubadilisha muundo wa ufundishaji, zana za kidijitali, na mifumo ya elimu inayozingatia mazingira. 

Wanafunzi wakisoma vitabu vyao darasani katika shule moja huko Phnom Penh, Cambodia.
© UNICEF/Bunsak But
Wanafunzi wakisoma vitabu vyao darasani katika shule moja huko Phnom Penh, Cambodia.

Ni wakati wa kutimiza ahadi kwa vitendo 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba “Sasa ni wakati wa nchi zote kutafsiri ahadi zao za mkutano huo katika hatua madhubuti zinazounda mazingira ya kusomea yenye kuunga mkono na kujumuisha wanafunzi wote. Sasa pia ni wakati wa kukomesha sheria na desturi zote za kibaguzi zinazozuia upatikanaji wa elimu.” 

Na kisha akaigeukia serikali ya Afghanista “Ntoa wito kwa mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan hasa kubadili marufuku ya kusitisha kupata elimu ya sekondari na ya juu kwa wasichana.” 

Pia amezihimiza nchi zote kuweka elimu katika kiini cha maandalizi ya mkutano wa malengo ya maendeleo endelevu SDG’s utakaofanyika mwaka huu  2023 na mkutano wa “mustakbali” utakaofanyika mwaka 2024. 

Zaidi ya yote, Bwana Guterres ameziomba asasi za kiraia na vijana kuendelea kutoa wito wa uwekezaji zaidi na bora kwa ajili ya upatikanaji wa elimu bora. 

Amehitimisha ujumbe wake kwa kuhimiza kwamba “Hebu tuache moto wa mabadiliko uendelee kuwaka.Wacha tutoe mifumo ya elimu ambayo inaweza kusaidia jamii kwa usawa, uchumi unaobadilika na ndoto zisizo na kikomo za kila mwanafunzi duniani.”