Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 40 ya wanafunzi duniani kote hawana fursa ya kusoma kwa lugha mama: UNESCO

Elimu kwa lugha mama huwezesha wanafunzi kuziba pengo ya maisha kati ya nyumbani na shuleni.
UNISFA
Elimu kwa lugha mama huwezesha wanafunzi kuziba pengo ya maisha kati ya nyumbani na shuleni.

Asilimia 40 ya wanafunzi duniani kote hawana fursa ya kusoma kwa lugha mama: UNESCO

Utamaduni na Elimu

Elimu itolewayo kwa wanafunzi kupitia lugha mama ikielezwa kuwa ni muhimu sio tu katika kuwezesha mtu kustawi na kuendelea bali pia kuhamisha urithi wa lugha, asilimia 40 ya wanafunzi duniani kote bado hawana fursa ya kufundishwa darasani kwa lugha yao wanaozungumza au wanaoelewa zaidi, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay katika ujumbe wake wa siku ya lugha mama duniani hii leo.

Amesema hali hiyo inadumaza kujifunza, kujieleza kitamaduni na kujenga mahusiano ya kijamii na vile vile kudhoofisha urithi wa lugha na hivyo amesmea ni muhimu suala la lugha mama lipatiwe kipaumbele katika marekebisho ya mfumo wa elimu. 

Mauthudi ya siku ya lugha mama mwaka huu ni “elimu kwa lugha mbalimbali ni lazima katika kurekebisha mfumo wa elimu” ikienda sanjari na mapendekezo yaliyotolewa wakati wa mkutano wa kimataifa wa marekebisho ya elimu mwaka jana ambapo msisitizo uliwekwa katika elimu na lugha za watu wa asili.

Elimu kwa lugha mbalimbali huchangia ujumuishwaji

Kwa mujibu wa UNESCO elimu inayotolewa kwa lugha nyingi ambayo hutokana na lugha mama hurahisisha ufikiaji na ujumuishwaji katika kujifunza kwa makundi ya watu wanaozungumza lugha zisizo za utawala, lugha za makundi madogo na lugha za asili.

Shirika hilo linasema sharti hili kwanza linahitaji ukusanyaji bora wa takwimu, ambazo zitafanya iwezekane kuchukua hatua maalum.

Zaidi ya yote, hata hivyo,UNESCO inasema inahitaji ufahamu wa jumla zaidi wa thamani isiyoweza kubadilishwa lakini dhaifu ya lugha na tamaduni mbalimbali ulimwenguni.

Shirika hilo limeendelea kusema kwamba “kila moja ya lugha zaidi ya 7,000 zinazozungumzwa na wanadamu hubeba ndani yake mtazamo wa kipekee wa ulimwengu, wa vitu na viumbe, njia ya kufikiri na hisia kiasi kwamba kila kutoweka kwa lugha kunaleta hasara isiyoweza kurejeshwa.”

Wasichana kutoka jamii ya watu wa asili wakipumzika na kusoma vitabu vyao nje ya Shule ya Mameya ya Ban Pho Wilayani Bak Hän ulioko katika Mkoa wa Remot Li Kai, Vietnam.
UNICEF/UNI10236/Estey
Wasichana kutoka jamii ya watu wa asili wakipumzika na kusoma vitabu vyao nje ya Shule ya Mameya ya Ban Pho Wilayani Bak Hän ulioko katika Mkoa wa Remot Li Kai, Vietnam.

Muongo wa kimataifa wa lugha za asili

Katika muktadha huu, muongo wa kimataifa wa lugha za asili (2022–2032), ambao UNESCO ndiyo shirika linalouongoza, ni fursa muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuhamasishwa ili kulinda sehemu kubwa ya tamaduni,mbalimbali duniani.

Hili pia ndilo dhumuni la siku hii ya kimataifa ya lugha mama limesema shirika la UNESCO, “kusherehekea njia za kueleza ulimwengu katika wingi wake, kujitolea kuhifadhi lugha mbalimbali kama urithi wa pamoja, na kufanya kazi kwa elimu bora katika lugha mama kwa wote.”

Siku ya kimataifa ya lugha mama inatambua kwamba lugha na wingi wa lugha vinaweza kuendeleza ushirikishwaji, na malengo ya maendeleo endelevu SDGs ya kutomwacha mtu yeyote nyuma.

UNESCO inahimiza na kuchagiza elimu kwa lugha mbalimbali kulingana na lugha mama au lugha ya kwanza.

“Ni aina ya elimu inayoanzia katika lugha ambayo mwanafunzi huimiliki zaidi na kisha kutambulisha lugha nyingine hatua kwa hatua. Mbinu hii huwawezesha wanafunzi ambao lugha yao mama ni tofauti na lugha ya kufundishia ili kuziba pengo kati ya nyumbani na shuleni, kugundua mazingira ya shule katika lugha iliyozoeleka, na hivyo, kujifunza vizuri zaidi.”

Siku ya kimataifa ya lugha mama huadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Februari.