Wanawake wa Kandahar wataka elimu ipewe kupaumbele

19 Februari 2018

Wanawake wa jimbo la Kandahar nchini Afghanistan wamesema elimu ndio jambo muhimu zaidi wanalohitaji ili kujikwamua.

Wamesema hayo katika mjadala  uliofanyika jimboni  humo na kuandaliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa  nchini Afghanistan, UNAMA.

Katika mjadala huo wanawake walipewa nafasi ya kujadili vikwazo vinavyokwamisha maendeleo yao katika nchi hiyo ambayo inakabiliwa na tatizo la usawa wa kijinsia.

Miongoni mwao Mariam Durani, ambaye ni mkereketwa wa haki za wanawake nchini Afghanistan amesema japo wanahitaji amani, usalama na maendeleo kiuchumi, bado ni dhahiri kwamba wanawamke wana haki ya msingi ya kupata elimu kama ilivyo kwa wanaume nchini humo.

Naye Dkt. Aziza ambaye ni mjumbe wa kamati ya amani ya jimbo la Kandahar amesema ukosefu wa elimu kwa wanawake vijijini umekithiri sana kwasababu wasichana wanaosoma hulazimishwa na wazazi wao waache shule kutokana na mila potofu.

UNAMA imekuwa ikishirikiana na asasi za kiraia na vyombo vya habari kwenye maeneo ya kusini mwa Afghanistan ili kupatia jamii fursa za kupaza sauti zao juu ya masuala yanayowaathiri.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter