Wataalamu wa UN wajiunga kutetea wananchi wa Zambia walioathiriwa na uchimbaji madini

Lango kuu la kuingia kwenye makao makuu ya ofisi ya haki za binadamu OHCHR mjini Geneva Uswis
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Lango kuu la kuingia kwenye makao makuu ya ofisi ya haki za binadamu OHCHR mjini Geneva Uswis

Wataalamu wa UN wajiunga kutetea wananchi wa Zambia walioathiriwa na uchimbaji madini

Haki za binadamu

Mahakama nchini Afrika Kusini imewaruhusu wataalamu wa Umoja wa Mataifa kushiriki kwenye kesi iliyofunguliwa na wananchi wa wilaya ya Kabwe nchini Zambia walioathirika na madini ya risasi kwenye uchimbaji wa madini uliofanywa na Kampuni ya madini ya Anglo American.

Kesi hiyo ya madai imefunguliwa kwa niaba ya watoto na wanawake walio katika umri wa kupata watoto ambao wamepata majeraha na madhara kutokana na kuathiriwa na madini ya risasi ambayo wanaeleza wameyapata kwenye miili yao kutokana na shughuli za uchimbaji madini zilizokuwa zinafanywa na kampuni hiyo.

Wiki hii Mahakama Kuu ya Gauteng Kusini itasikiliza hoja kuhusu iwapo kuna uhalali wa kuzingatia madai ya uharibifu ambayo waathiriwa wamewasilisha.

Taarifa iliyotolewa kutoka Geneva Uswisi imewanukuu wataalamu hao wakieeleza kuwa “kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, hakuna kiwango chochote cha kukumbwa na madini hayo ya risasi ambacho kinajulikana kutokuwa na madhara. Watoto wadogo wanaweza kupata madhara makubwa na ya kudumu ya afya na ulemavu, ikiwa ni pamoja na katika ukuaji wa ubongo na mfumo wa neva. Wanawake wajawazito kuwa katika hatari ya kupata madini ya risasi inaweza kusababisha kuharibika kwa mimba, watoto kupoteza maisha wakuwa tumboni, na kuzaliwa kabla ya wakati na kuzaliwa kwa uzito mdogo.”

Kulikoni kesi ya wazambia kufunguliwa Afrika Kusini?

Kesi hiyo ya wananchi wa Zambia iliwasilishwa nchini Afrika Kusini dhidi ya kampuni ya Anglo American kwa kuwa makao yake makuu yapo nchini humo.

Mahakama itazingatia hoja zinazotokana na sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kanuni elekezi za Biashara na Haki za Kibinadamu zinazotaka makampuni ya biashara kuheshimu haki za binadamu, kuelekeza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuepuka kukiuka haki za binadamu za wengine, wakati wakishughulikia haki za binadamu, athari zinazohusishwa na shughuli za biashara ambazo wanahusika nazo, na kuangazia umuhimu wa kufikia suluhu endapo kuna ukiukwaji.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa ambao katika kesi hiyo watashiriki katika kutoa elimu na taarifa za kitaalamu za haki za binadamu, walidai kuwa Anglo American ilikuwa ikifanya kinyume na ahadi yake ya kutekeleza haki za binadamu katika biashara, wakati inapinga Mahakama hata kuzingatia hatua hii ya awali ya kesi hiyo

“Kampuni ya Anglo American Afrika Kusini imejitolea kwa hiari kufuata Kanuni elekezi, ikiwa ni pamoja na dhamira ya kusaidia upatikanaji wa haki pale ambapo athari za haki za binadamu zimetokea na kushirikiana katika michakato iliyoundwa ili kubaini kama kuna hatia ya athari hizo," wameeleza wataalam hao.

Kuhusu madini ya risasi

Madini ya risasi yanayotambulika kwa kiingereza kama “Lead” ni sumu iliyojikusanya ambayo huathiri mifumo mingi ya mwili na ni hatari kwa watoto wadogo.

WHO imeibainisha kuwa ni miongoni mwa kemikali 10 zinazosumbua sana afya ya jamii, zinazohitaji kuchukuliwa hatua na nchi wanachama kulinda afya za wafanyakazi, watoto na wanawake walio katika umri wa kupata watoto.