Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madini ya risasi yaendelea kuathiri mustakabala wa watoto- UNEP

Piga marufuku rangi zenye madini ya risasi
UNEP
Piga marufuku rangi zenye madini ya risasi

Madini ya risasi yaendelea kuathiri mustakabala wa watoto- UNEP

Afya

Pale unapopaka rangi ili kupendezesha kuta za nyumba kumbe ndio unahatarisha maisha ya mtoto wako. Je wajua ni kwa njia gani?

Wiki ya kuelimisha umma juu ya athari za matumizi ya madini ya risasi kwenye rangi ikiwa inaendelea, shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP limesema kuendelea kuwepo kwa madini  hatari ya risasi kwenye rangi za nyumba kunatishia afya ya watoto.

Katika makala maalum iliiyopatiwa jina, risasi na mustakabali hatari kwa watoto, UNEP inasema miaka kadhaa tangu madini hayo ya risasi yapigwe marufuku kutumika kwenye rangi za nyumba na petroli.

Madini ya risasi yana sumu ambayo inaweza kumpata mtoto akiwa bado tumboni mwa mama yake na hata athari za maisha yote ikiwemo kushindwa kujifunza, ukosefu wa damu, kutokuona vyema na kushindwa kuzungumza.

Jacob Duer, ambaye ni mkuu wa kitengo cha kemikali na afya UNEP amesema “madini ya risasi hupatikana kwenye rangi za kupaka  ndani ya nyumba, shule, majengo ya umma na hata kwenye vikaragosi wanavyochezea watoto, maeneo ya kuchezea watoto pamoja na samani.

Akifafanua madhara ya madini ya risasi kwa watoto, Profesa Monebenimp wa Chuo Kikuu cha Tiba huko Yaounde nchini Cameroon amesema,

(Sauti ya Profesa Francisca Monebenimp)

Utafiti wetu umebaini kuwa zaidi ya asilimia 88 ya watoto wana zaidi ya mikrogramu 5 ya madini ya risasi kwenye kila lita ya damu mwilini. Je kwa nini hili ni muhimu? Kwa sababu sasa tunaweza kufahamu tatizo lipo na tunaweza kuelimisha vyema jamii.  Familia zilizoshiriki utafiti huu zimetambua kuwa ni lazima kuchukua hatua dhidi ya mazingira.Ni kwa sababu hivi sasa watu wana wasiwasi na hivyo tunaweza kuelimisha watu kwa kutumia takwimu hizi."

Utafiti unaonyesha kuwa madini ya risasi yaliyowekwa kwenye rangi za kuta yanaanza kuwa na madhara pindi rangi hiyo inapoanza kubanduka.

Ripoti ya UNEP inaonyesha kuwa idadi kubwa ya rangi za kupendezesha nyumba bado zina kiwango kikubwa cha madini ya risasi na hadi sasa ni nchi 69 tu zimeridhia sheria dhidi ya madini hayo kutumika kwenye rangi.

Shirika la afya ulimwenguni WHO linatoa wito kwa sekta binafsi kuchukua hatua kuondokana na rangi hii ikielezwa kuwa gharama ya kuondokana na madini hayo ni ndogo ikilinganishwa na madhara ya kiafya na kimazingira.

Wiki ya kuhamasisha umma kuhusu athari za matumizi ya madini ya risasi ilianza tarehe 21 mwezi huu wa Novemba na itakamilika tarehe 27 mwezi huu.