Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kudorora kwa uchumi kunaweza kulazimisha watu kukubali kazi zisizo na staha: ILO

Vijana wa kike wakifungasha maharagwe kwenye shamba mjini Addis Ababa, Ethiopia.
© ILO/Sven Torfinn
Vijana wa kike wakifungasha maharagwe kwenye shamba mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kudorora kwa uchumi kunaweza kulazimisha watu kukubali kazi zisizo na staha: ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Kudorora kwa ukuaji wa ajira duniani na shinikizo la mazingira mazuri ya kazi vinahatarisha kudhoofisha haki ya kijamii, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa duniani ILO.

Ripoti hiyo “Mwelekeo wa ajira duniani na mtazamo wa kijamii mwaka 2023.” kudorora kwa sasa kwa uchumi wa dunia kuna uwezekano wa kulazimisha watu zaidi kukubali ajira za ubora wa chini, kazi zinazolipwa vibaya ambazo hazina usalama wa kazi na ulinzi wa kijamii, na hivyo kuzidisha ukosefu wa usawa unaochangiwa na janga la COVID-19.  

Ripoti imeendelea kusema kwamba soko la ajira mwaka huu wa 2023 litaporomoka kwa asilimia 1.0% ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.3% mwaka 2022.  

Mkwamo katika kujikwamua na COVID-19 

Kiwango hili cha mgogoro wa ajira itakwamisha pia kujikwamua vyema na janga la COVID-19 ambako tayari hakuna usawa na hakujakamilika katika maeneo mengi duniani.  

ILO inasema pia “Mgogoro wa gharama za maisha pia unatishia uwezo wa watu kuishi na utazidisha kusuasua kwa uundaji wa fursa za ajira na hiyo kupanua pengo la ukosefu wa ajira duniani ambalo mwaka huu linatarajiwa kuongezeka kwa watu milioni 3 na kufikia zaidi ya watu milioni 208 wasio na ajira kote duniani.”  

Ripoti imeongeza kuwa ukubwa wa wastani wa ongezeko hili linalotarajiwa kwa kiasi kikubwa unatokana na upungufu wa nguvu kazi katika nchi zenye kipato cha juu.  

Hii itaashiria mabadiliko ya kupungua kwa ukosefu wa ajira duniani kote yaliyoshuhudiwa kati ya 2020-2022.  

Na ina maana kwamba ukosefu wa ajira duniani utasalia kuwa milioni 16 juu ya kiwango cha kabla ya mgogoro wa COVID-19 uliozuka 2019. 

Baba asiye na ajira akipokea msaada kutoka UNICEF nchini Afghanistan.
© UNICEF/Omid Fazel
Baba asiye na ajira akipokea msaada kutoka UNICEF nchini Afghanistan.

Wafanyakazi wengi wako katika uchumi usiorasmi 

Ripoti hiyo ya mwenendo wa ajira 2023 inasema hadi sasa kuna wafanyakazi bilioni 2 wako katika mfumo wa uchumi usio rasmi, bila mikataba wala marupurupu yoyote huku wengine milioni 214 wakiishi katika umasikini mkubwa licha ya kuwa na ajira.  

Waathirika wakubwa wa hali hii kwa mujibu wa ripoti ni vijana na wanawake.  

Wakati huo huo ripoti imesisitiza kwamba “fursa finyu za ajira, ulinzi duni wa hifadhi ya jamii, na kunyimwa haki kazini, vinaendelea kuwa changamoto kubwa hasa kwa kuzingatia kuwa ajira zenye staha ni nguzo ya haki za kijamii.”  

Ripoti hiyo pia inabainisha hatua mpya, za kina za hitaji lisilofikiwa la ajira na pengo la ajira duniani.  

Pamoja na wale ambao hawana ajira, hatua hii inajumuisha pia watu wanaotaka kuajiriwa lakini hawatafuti kazi kwa bidii, ama kwa sababu wamekata tamaa au kwa sababu wana majukumu mengine kama vile majukumu ya utunzaji wa wapendwa wao.  

Pengo la ajira duniani lilikuwa watu milioni 473 mwaka 2022, ikiwa ni karibu watu milioni 33 juu ya kiwango cha mwaka  2019.