Skip to main content

Athari za COVID-19 kwa vijana zinatishia nguvu kazi ya kizazi hicho:ILO

Mfanyakazi wa kufyatua mtofali akiwa mahali pa kazi ya ujenzi ..
ILO/Apex Image
Mfanyakazi wa kufyatua mtofali akiwa mahali pa kazi ya ujenzi ..

Athari za COVID-19 kwa vijana zinatishia nguvu kazi ya kizazi hicho:ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO imesema athari mbaya za janga la corona au COVID-19 kwa vijana zimeongeza pengo la usawa na kuhatarisha uwezo wa uzalishaji wa kizazi hicho chote katika jamii.

Ripoti hiyo “Vijana na COVID-19, athari katika ajira, elimu, haki na afya ya akili” iliyotolewa Jumatano wiki hii inaonyesha kwamba janga la COVID-19 lina athari kubwa katika elimu na mafunnzo kwa vijana.  

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya video wakati wa utoaji wa ripoti hiyo mjini Geneva Uswisi Susana Puerto Gonzalez mtaalam wa ILO wa masuala ya utafiti na ajira kwa vijana amesema   “Licha ya juhudi kubwa kutoka katika shule na taasisi za mafunzo katika kuhakikisha elimu inaendelea kupitia masomo mtandaoni, mwanafunzi 1 kati ya wa 8 hawakupata fursa ya masomo hususan kwa vijana kutoka nchi za kipato cha chini na pia kuongeza pengo la kidijitali miongoni mwa kanda mbalimbali.”

Ripoti hiyo ya ILO inasema tangu kuanza kwa janga la COVID-19 zaidi ya asilimia 70 ya vijana ambao wanasoma au wanaosoma na kufanya kazi wameathirika kwa sababu ya kufungwa shule, vyuo na vituo vya mafunzo.  

Na kuhusu suala la ajira Bi Gonzales amesema ripoti inaonyesha kwamba kijana 1 kati ya 6 ameacha kufanyakazi tangu kuzuka kwa virusi hivyo na kwamba"Asilimia 70 ya vijana huenda wameathirika na taharuki na msongo wa mawazo.”  

Na kwa mantiki hiyo amesema ILO inatoa wito wa hatua za haraka ikiwemo uwekezaji katika ajira ya vijana ili kuweza kuwasaidia vijana kwa usalama kipindi hiki cha mpito hasa katika uzalishaji wa ajira na kazi zenye tija.