Wanawake na wanaume wakiwa sawa katika soko la ajira pato la dunia lipanda zaidi ya  asilimia 25:UNIDO

3 Septemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO, limesema endapo wanawake watapatiwa fursa sawa na wanaume katika soko la ajira basi pato la dunia litaongezeka kwa zaidi ya asilimia 25 ifikapo mwaka 2025.

Katika taarifa yake iliyotolewa mapema wiki hii UNIDO ikizichagiza nchi kuwapa nafasi zaidi za kiuchumi wanawake imesema, ”kuwawezesha wanawake ndio njia pekee ya kusonga mbele kwani ili uchumi ukue kwa kasi , idadi ya watu masikini ipungue na ustawi wa watu uboreke inahitaji wanaume na wanawake kuwa sawa”. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa ili kufikia lengo hilo ambalo ni chachu ya kutimiza ajenda ya malengo ya maendeleo ya 2030 au SDGs, UNIDO imeweka mikakati ya masuala ya jinsia katika programu, sera na miradi yake. 

Lengo kuu la kufanya hivyo ni, “kuimarisha ujumuishwaji wa wanawake na kuleta maendeleo ya viwanda.” 

Kwa kushirikiana na wadau wengine wa Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia na umma, UNIDO inaandaa ushirikiano wa shughuli za kiufundi, ili kuchagiza uwekezaji katika biashara zinazoendeshwa na kumilikiwa na wanawake , kuimarisha mitandao ya wanawake , kuboresha fursa za masoko, na kutoa mafunzo ya teknolojia na suluhu ya nishati safi inayojali mazingira. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kukumbatia uwezo wa wanawake kunachangia kuleta maendeleo ya viwanda na kuongeza pato la ndani hivyo “Ukuaji wa pato la ndani la dunia utaongezeka kwa asilimia zaidi ya 25% ifikapo mwaka 2025 endapo wanawake watakuwa na jukumu sawa na wanaume katika soko la ajira.” 

Kwa mantiki hiyo UNIDO imesisitiza kwamba kwa kuboresha hadhi na kipato cha wanawake kwa kila nchi “sio tu tunaboresha hadhi na ustawi wao bali tunaboresha maisha yetu sote.” 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter