Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu bil 1 wanapata huduma kwenye vituo vya afya visivyo na umeme wa uhakika

Mama akiwa amembeba mwanae mwenye umri wa miezi mitatu wakati anapatiwa chanjo dhidi ya Surua kwenye kituo cha afya jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
© UNICEF/Karel Prinsloo
Mama akiwa amembeba mwanae mwenye umri wa miezi mitatu wakati anapatiwa chanjo dhidi ya Surua kwenye kituo cha afya jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Takriban watu bil 1 wanapata huduma kwenye vituo vya afya visivyo na umeme wa uhakika

Afya

Takriban watu bilioni moja duniani kutoka nchi zenye kipato cha chini na cha kati wanapatiwa huduma za afya katika vituo vya afya visivyo na umeme wa uhakika, hii ikimaanisha ni uwiano wa mtu 1 kati ya watu 8 wanapata huduma za afya katika vituo visivyo na umeme wa uhakika.

Hayo yapo kwenye ripoti ya pamoja ya mashirika manne ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi iliyopewa jina la Nishati katika Afya: Kuongeza Upatikanaji wa Umeme katika Vituo vya Huduma za Afya ambayo imeeleza kuwa bila kuwa na umeme wa uhakika katika vituo vya afya lengo la Huduma ya Afya kwa wote haliwezi kufikiwa na kuzitaka nchi zote duniani kuhakikisha wanaweka umeme vituoni ili kuweza kuoka maisha ya watu.

Mashirika hayo Ya Umoja wa Mataifa yaliyotoa ripoti hiyo ya pamoja ni lile la Afya Ulimwenguni WHO, la nishati jadidifu, IRENA, Benki ya Dunia, na Nishati Endelevu kwa Wote (SEforAll).

Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO anayehusika na kitengo cha Watu wenye Afya Bora Dkt. Maria Neira amesema upatikanaji wa umeme katika vituo vya huduma za afya unaweza kuleta tofauti kati ya maisha na kifo. “Kuwekeza katika nishati ya kuaminika, safi na endelevu katika vituo vinavyotoa huduma ya afya sio tu muhimu kwa utayari wama janga, bali pia unatajika ili kufikisa lengo la afya kwa wote, pamoja na kuongeza ustahimilivu pamoja na mnepo wa mabadiliko ya tabianchi.”

Sedelia Abdullahi ni mhudumu wa afya wa mstari wa mbele huko mashinani nchini Ethiopia na kila siku huchunguza na kutibu watoto wenye utapiamlo kwenye kituo cha afya cha kambi ya wakimbizi ya Bambassi nchini Ethiopia kilichojengwa na UNICEF kwa ufadhili …
UNICEF Ethiopia
Sedelia Abdullahi ni mhudumu wa afya wa mstari wa mbele huko mashinani nchini Ethiopia na kila siku huchunguza na kutibu watoto wenye utapiamlo kwenye kituo cha afya cha kambi ya wakimbizi ya Bambassi nchini Ethiopia kilichojengwa na UNICEF kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya.

Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika hali mbaya

Nusu ya vituo vya afya Kusini mwa jangwa la Sahara havina umeme wa kutegemewa hata kwa nusu ya vituo vyake vya afya.

Ingawa kumekuwa na maendeleo katika miaka ya hivi karibuni katika usambazaji wa umeme kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, takriban watu bilioni 1 kote ulimwenguni wanahudumiwa na vituo vya kutolea huduma za afya bila ya kuwa na umeme wa kutegemewa au bila ya kuwa na umeme kabisa.

Hii ni sawa na karibu watu wote wanaoishi katika nchi za Marekani, Indonesia, Pakistan na Ujerumani.

Vituo vingi vya afya vinavyokosa umeme ni vya vijijini ikilinganishwa na vituo vya afya vya mijini.

Kwakuwa huduma ya afya ni haki ya msingi ya kila binadamu ndio maana serikali na wadau wote wanahimizwa kuwekeza katika kutafuta suluhu mbalimbali za kupata umeme na kwakutumia nishati endelevu kama vile umeme wa nguvu ya jua au Sola.

Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya
UNOCHA/Giles Clarke
Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya

Kilichopo kwenye ripoti

Uwekezaji katika upatikanaji wa umeme ni jambo kubwa litakalo fanikisha kufikia lengo la cha Huduma ya Afya kwa Wote, ripoti hiyo inasema, na hivyo hivyo uwekaji umeme kwenye vituo vya huduma ya afya lazima kuzingatiwa kuwa kipaumbele cha juu cha maendeleo kinachohitaji usaidizi mkubwa na uwekezaji kutoka kwa serikali, wadau wa maendeleo na mashirika ya ufadhili na maendeleo.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa mahitaji uliofanywa na Benki ya Dunia uliojumuishwa katika ripoti hiyo, karibu theluthi mbili, sawa na 64% ya vituo vya huduma za afya katika nchi za kipato cha chini na cha kati vinahitaji usaidizi wa haraka wa ama kuweka mifumo ya umeme au kurekebisha mifumo duni iliyopo  ambayo inahitaji haraka takriban dola 4.9 ili angalau waweze kufikia katika kiwango kidogo cha usambazaji wa umeme.

Umeme katika vituo vya Afya

Ni muhimu kuwa na umeme kwa ajili ya taratibu za kawaida na za dharura.

Umeme unahitajika katika vituo vya afya ili kuwasha vifaa vya msingi zaidi kuanzia taa, vifaa vya mawasiliano, friji, mpaka vifaa vinavyotumika kupima ishara muhimu kama vile mapigo ya moyo na shinikizo la damu.

Wakati vituo vya afya vikiwa na vyanzo vya nishati vinavyotegememewa, vifaa muhimu vya matibabu vinaweza kuwashwa na kufungwa, zahanati zinaweza kuhifadhi chanjo za kuokoa maisha, na wafanyakazi wa afya wanaweza kufanya upasuaji muhimu au wanawake kujifungua watoto kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, katika ukanda wa nchi za Kusini mwa bara la Asia na nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ripoti imebaini zaidi ya vituo vya afya 1 kati ya 10 vinakosa huduma yoyote ya umeme.