Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Ikiwa dunia inataka kupambana na mabadiliko ya tabianchi, njia ni kuhamia katika nishati jadidifu

Modera inanufaika kutoka kwa kiwanda cha nguvu cha Megawati 6 kilichowekwa katika kijiji cha karibu cha Sujjanpura.
UN News
Modera inanufaika kutoka kwa kiwanda cha nguvu cha Megawati 6 kilichowekwa katika kijiji cha karibu cha Sujjanpura.

Guterres: Ikiwa dunia inataka kupambana na mabadiliko ya tabianchi, njia ni kuhamia katika nishati jadidifu

Tabianchi na mazingira

Mkutano Mkuu wa 13 wa Shirika la kimataifa la nishati jadidifu, IRENA umeanza rasmi hii leo huko Abu Dhabi nchini Falme za Kiarabu UAE ambapo umewaleta pamoja wakuu wa nchi, Mawaziri na watoa maamuzi wa masuala ya nishati kutoka mashirika ya kimataifa, wadau wa kimataifa na wahusika binafsi lengo likiwa ni kutathmini maendeleo na kuainisha ajenda za utekelezaji ili kuharakisha mchakato wa dunia kuhamia katika matumizi ya nishati jadiifu.

Akizungumza katika mkutano huo kwa njia ya Video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ikiwa dunia inataka uondokana na athari za mabadiliko ya tabianchi basi njia ya kufanya ni kuhamia katika matumizi ya nishati jadidifu na kutoa wito kwa wadau wote duniani kuongeza mara mbili uwekezaji wa nishati hiyo katika gridi za umeme ifikapo mwaka 2030.

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza haja ya kupunguza gharama za mtaji kwenye nishati jadidifu na kuhakikisha kuwa ufadhili unawafia wale waliona uhitaji zaidi.

Guterres ameeleza kuwa dunia inaendelea kutumia nishati ya mafuta ya kisukuku ilihali nyuzi joto sasa inaenda kufikia 1.5 selsiasi na kueleza kuwa iwapo dunia itaendelea na matumizi hayo baada ya muongo mmoja nyuzi joto itakuwa 2.8 katika vipimo vya selsiasi.

Paneli za solar, Nevada, California.
© BLM Nevada
Paneli za solar, Nevada, California.

Guterres ameeleza nini kifanyike ili kuwezesha dunia kuhamia kwenye matumizi ya nishati mbadala na kuachana na nishati ya mafuta ya kisukuku ikiwa dunia inataka kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, " Mosi, lazima tuondoe vizuizi vya uvumbuzi na tubadilishane teknolojia muhimu zinazoweza kuleta manufaa na jumuishi ili ziwe bidhaa za umma za kimataifa. Pili, lazima tubadilishe na kuongeza ufikiaji wa minyororo ya usambazaji wa malighafi na vipengee vya teknolojia zinazoweza kurejeshwa, bila kuharibu mazingira yetu. Hii inaweza kusaidia kuunda mamilioni ya kazi zinazojali utunzaji wa mazingira, haswa kwa wanawake na vijana katika nchi zinazo endelea."

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameendelea kwa kutaja mambo mengine kuwa ni " Tatu, watoa maamuzi lazima wakate utepe mwekundu, kuidhinisha haraka miradi endelevu duniani kote na wafanye gridi za umeme kuwa za kisasa. Nne, ruzuku ya nishati lazima iondoke kutoka kwa mafuta hadi nishati safi na ya bei nafuu. Na lazima tuunge mkono vikundi vilivyo hatarini vilivyoathiriwa na mabadiliko haya. na tano, uwekezaji wa umma na wa kibinafsi katika nishati jadidifu unapaswa kuongezeka mara tatu hadi angalau kufikia dola trilioni 4 kwa mwaka."

Kabla ya kumaliza hotuba yake aligusia pia suala la uwekezaji kwa usawa na kubainisha kuwa nchi nyingi zinazoendelea hazina uwekezaji mkubwa kwenye nishati jadidifu na moja ya sababy ni gharama akieleza kuwa bei ya teknolojia mbadala inaweza kuwa mara saba zaidi katika nchi zinazoendelea.

Mkutano huo wa mwaka ambao unafanyika kwa siku mbili umewakutanisha zaidi ya washiriki 1,500 chini ya kauli mbiu isemayo “Mabadiliko ya Nishati Duniani:Mwitikio wa kidunia” ambapo kwa siku mbili wadau watajadili na kubainisha vipaumbele vya mpito wa nishati ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Fundi akirekebisha mambo kwenye mtambo wa sola nchini Thailand
© ADB

PGA na Mapendekezo ya nini kifanyike

Akiunga mkono kile kilichoelewa na Katibu Mkuu, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi amesema nchi zote zinaweza kuamua kupunguza utegemezi kwenye mafuta ua kisukuku na kuamua kuhamia katika nishati jadidifu ambayo itasaidia kuleta uwiano duniani.

Na ili uwiano uweze kufikiwa Kőrösi ametoa mapendekezo matatu ambayo ni “Mosi, kuwekeza katika zana za kisayansi zinazoweza kupimika, hii ikijumuisha uundaji wa utaratibu wa kufuatilia ili kutathmini ni wapi tunaelekea, na wapi tunabaki nyuma. Mbili, ili kuharakisha mpito na kufanya nishati mbadala kuwa na manufaa kwa umma duniani kote, sote lazima tushirikishane maarifa yetu, na kuhamisha teknolojia zetu. Tunapaswa kufanya kazi pamoja ili kufanya utawala wa haki miliki kuwezesha mpito wa nishati na uvumbuzi, na sio kizuizi kwenye hili.”

Rais huyo wa Baraza la Umoja wa Mataifa ametaja sababu ya tatu kuwa “Tunapaswa kuimarisha ushirikiano na wadau, kuanzia wasomi hadi raia kupitia makampuni, ambao wana rekodi nzuri katika mipango endelevu ya nishati”.

Rais wa Mkutano Mkuu wa 13 wa IRENA

“Tuna fursa nzuri na wajibu wa kuhakikisha kwamba maamuzi ya nishati ya leo yanatuweka katika mwelekeo mzuri wa maendeleo endelevu.” Amesema Mkurugenzi Mkuu wa IRENA Francesco La Camera na kuongeza kuwa “Mkutano huu pamoja na mambo mengine unawezesha serikali kuoanisha juhudi zao za ujenzi wa mfumo mpya wa nishati, kufikia mafanikio ya Malengo ya Mkataba wa Paris na kutimiza vipaumbele muhimu vya juu zaidi kimataifa kama vile uundaji wa nafasi za kazi, maendeleo ya viwanda rafiki kwa mazingira na minyororo ya usambazaji, usalama wa nishati na ufikiaji wa ulimwengu wote.”

Kwa upande wake Rais mteule wa Mkutano huu wa 13 wa IRENA ambaye pia ni Waziri wa nishati wa India Raj Kumar Singh amesema mabadiliko ya nishati sio tu kipaumbele katika nyakati hizi lakini pia ni wajibu kwa nchi, viwanda, na jumuiya. “India inaendelea kuonesha juhudi zake za nguvu katika hili. Tunatazamia kuwezesha majadiliano ngazi za juu ya mwelekeo wa mpito wa nishati katika maandalizi ya mchakato wa wadau.”

Mkutano huo unahusisha majadiliano yenye lengo la kutafuta suluhisho zitakazo wezesha nchi kupita vyema kwenye mpito wa nishati kwa kuangalia mambo kama vile uwekezaji, nyenzo muhimu, upangaji wa nishati, uondoaji wa matumizi ya nishati inayotoa hewa ya kaboni na uhusiano wa hewa hiyo na huduma ya afya mbadala.