Doria mpya Ituri nchini DRC kufuatia mauaji na mashambulizi Jumapili
Doria mpya Ituri nchini DRC kufuatia mauaji na mashambulizi Jumapili
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umeendelea na doria mpya kwenye eneo la Roe-Drodro kwenye mji wa Djugu jimboni Ituri kufuatia mfululizo wa mashambulizi kutoka wanamgambo wa CODECO.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani akinukuu MONUSCO.
Amesema hali imedhibiti lakini bado ni tete wakati huu ambapo raia 18 waliuawa ambapo 17 kati yao waliuawa jumapili huku maelfu wakifurushwa na kusaka makazi kwenye kituo cha Roe jimboni Ituri.
Bwana Dujarric amenukuu pia MONUSCO ikisema licha ya waasi wa M23 kukabidhi kambi ya kijeshi ya Rumangabo iliyoko jimboni Kivu Kaskazini kwa jeshi la kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki, waasi hao wamesalia kwenye eneo la Jirani na wanaendeleza mashambulizi kwenye maeneo kadhaa kusini mwa mji wa Rutshuru, jimboni humo.
Kauli kuhusu tisho la Rwanda kufukuza wakimbizi wa DRC
katika mkutano huo, waandishi wa habari walimuuliza Bwana Dujarric kuhusu kauli ya Rais wa Rwanda Paul Kagame ya kutishia kufurusha maelfu ya wakimbizi wa DRC walioko Rwanda, ambapo amesema, “si suala kwamba tuna ujumbe wa UN, ni kwamba kila nchi mwanachama ana wajibu wa kuzingatia sheria ya kimataifa ya mkimbizi, katu asilazimishe watu wanaokimbia ghasia kurejea makwao na kuhakikisha kuwa wanapatiwa ulinzi na usalama na hilo linagusa nchi zote wanachama.”
Ameongeza kuwa “kikundi cha M23 kwa kadri tunavyofahamu, wanaendelea kuweko na kuna vikundi vingine na kwamba sehemu kubwa ya eneo hilo bado si salama kwa watu ambao watasaka usalama kokote pale wanakoweza.
M23 izingatia uamuzi wa Luanda wa kuondoka kabla ya 15 Januari
Bwana Dujarric amsema “ni lazima mamlaka za DRC, nchi za kikanda wakiwemo majirani wa DRC washirikiane kuhakikisha wananchi wa DRC wako salama na wanaweza kurejea nyumbani.
Amenukuu MONUSCO ikisisitiza wito wake kwamba M23 lazima wazingatie uamuzi uliopitishwa kwenye mkutano wa viongozi nchini Luanda wa kuondoka kwenye maeneo wanayokalia jimboni Kivu Kaskazini na kuelekea maeneo yaliyokubaliwa kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa mkutano wa Luanda na wanapaswa kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 mwezi huu wa Januari na wasitishe chuki.