Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunasikitishwa sana na hali tete ya usalama Mashariki mwa DRC. Wekeni silaha chini – Msemaji UN 

Wakimbizi wa ndani katika kambi ya Loda iliyoko Fataki jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/Roger LeMoyne
Wakimbizi wa ndani katika kambi ya Loda iliyoko Fataki jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Tunasikitishwa sana na hali tete ya usalama Mashariki mwa DRC. Wekeni silaha chini – Msemaji UN 

Amani na Usalama

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric hii leo mjini New York, Marekani amesema Umoja wa Mataifa unasikitishwa na kuzorota kwa hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

Dujarric amesema Umoja wa Mataifa unalaani ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia yanayofanywa na kikundi cha waasi kilichojipatia jina CODECO (cha wanamgambo waliojihami kutoka kabila la walendu huko Ituri) na M23 pamoja na kuwepo kwa makundi mengine ya kigeni yenye kujihami kwa silaha ikiwa ni pamoja na Allied Democratic Forces (ADF), Red Tabara na Forces Démocratique pour la libération de Rwanda (FDLR), ambayo yanaendelea kuwa tishio kwa utulivu wa kikanda. 

Msemaji huyo ameeleza pia kuwa Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa makundi yote yenye silaha kusitisha mara moja aina zote za vurugu. 

"Tunahimiza makundi yenye silaha ya Congo kushiriki bila masharti katika Mpango wa Kupokonya Silaha, Uvunjaji wa makundi, Mpango wa Kurejesha jamii katika hali yake na Uimarishaji (P-DDRCS), na makundi ya kigeni yenye silaha kuziweka silaha chini mara moja na kurejea katika nchi zao za asili.

Watoto wakimbizi wa ndani huko Ituri nchini DRC.
UN/Eskinder Debebe
Watoto wakimbizi wa ndani huko Ituri nchini DRC.

“Tunakaribisha na kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kisiasa za kitaifa na kikanda kuunga mkono upokonyaji silaha kwa makundi yenye silaha, ikiwa ni pamoja na Rais Félix Tshisekedi wa DRC na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kupitia mchakato wa Nairobi. MONUSCO pia inafanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mjumbe Maalumu wa UN wa eneo la Maziwa Makuu ili kuendeleza hatua zisizo za kijeshi za kupokonya silaha makundi ya kigeni yenye silaha.” Amesema Bwana Dujarric. 

Aidha Msemaji huyo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, wanakaribisha uteuzi wa Rais João Lourenço wa Angola na Umoja wa Afrika ili kutuliza mvutano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda. “Umoja wa Mataifa unaunga mkono kikamilifu juhudi hizi za kisiasa.” 

Huko Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, MONUSCO inawalinda raia bila upendeleo na kwa nguvu na kusaidia kukomesha makundi yenye silaha, kama ilivyoamrishwa na Baraza la Usalama. 

Katika kutekeleza jukumu lake la ulinzi wa raia, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO inaendelea kuhakikisha uungaji mkono wake kwa Jeshi la serikali ya DRC, FARDC unazingatia kikamilifu Sera ya Umoja wa Mataifa ya Kuzingatia Haki za Kibinadamu.

Wanavikosi wa MONUSCO wakipiga doria mkoa wa Ituri nchini DRC. (Maktaba)
MONUSCO
Wanavikosi wa MONUSCO wakipiga doria mkoa wa Ituri nchini DRC. (Maktaba)

Hii ni kuhakikisha kwamba msaada wa Ujumbe huo kwa vikosi vya usalama visivyo vya Umoja wa Mataifa unaendana na madhumuni na kanuni za Shirika kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa na wajibu chini ya sheria za kimataifa. 

Dujarric pia amesema wana wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kuongezeka kwa matamshi ya chuki nchini dhidi ya baadhi ya jamii fulani, ikiwa ni pamoja na katika muktadha wa kuzuka upya kwa M23. “Matamshi ya chuki lazima yakabiliwe kwa umakini.”