Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waasi wa M23 waondoke haraka maeneo waliyotwaa DRC- Baraza la Usalama UN

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini. (MAKTABA)
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini. (MAKTABA)

Waasi wa M23 waondoke haraka maeneo waliyotwaa DRC- Baraza la Usalama UN

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali kurejea upya kwa mashambulizi yanayofanywa na waasi wa kikundi cha M23 huko jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kitendo cha waasi hao kuendelea kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa jimbo hilo, Goma na maeneo mengine.

Kauli ya wajumbe hao imo kwenye taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Baraza hilo kufuatia kikao chake ambamo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita aliwapatia taarifa ya kile kinachoendelea DRC.

Wajumbe hao wamelaani pia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama na utulivu kwenye ukanda wa Maziwa Makuu na kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama.

“Tunataka sitisho mara moja la chuki na kukoma kwa kitendo cha M23 kuendelea kusonga mbele, na wakati huo huo kikundi hicho kiondoke kwenye maeneo ambayo kimeyatwaa na kuyashikilia,” imesema taarifa hiyo bila kutaja maeneo yaliyotwaliwa na M23 nchini DRC.

Tunaunga mkono juhudi za kiusalama la kikanda

Wajumbe hao pia wamesisitiza kuunga mkono hatua za kikanda zilizochukuliwa na kwa mujibu wa Mpango wa Amani, Usalama na Ulinzi kwa ajili ya DRC na vile vile kitendo cha ukanda huo kutovumilia na vile vile kutosaidia vikundi vilivyojihami.

“Tunatoa wito wa kusitishwa kwa msaada wowote ule wa kigeni kwa vikundi visivyo vya kiserikali likiwemo kundi la M23.”

Mwanamke mkimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, akiwa kambini Kanyaruchinya baada ya kukimbia makazi  yake kutokanana mapigano kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23
UN
Mwanamke mkimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, akiwa kambini Kanyaruchinya baada ya kukimbia makazi yake kutokanana mapigano kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23

Baraza la Usalama pia limeleza hofu yake kubwa kuhusu ongezeko la idadi ya wakimbizi wa ndani na wakimbizi na kutoa wito kwa pande husika kwenye mzozo hususan kikundi cha M23 kuruhusu kwa mujibu wa sheria za kimataifa ikiwemo ya haki za binadamu na ile ya msaada wa kibinadamu, ufikishaji wa misaada ya kiutu halikadhalika kuepuka kushambulia raia.

Kwa jumuiya ya kimataifa, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameisihi  iongeze msaada wake kwa serikali ya DRC kwa kutatua mzozo wa kiutu na kupeleka msaada wa kibinadamu.

Tunapongeza mchakato wa Nairobi kupitia EAC

Mchakato wa amani na usalama DRC kupitia Mchakato wa Nairobi unaosongeshwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, nao umepigiwa chepuo ambapo wajumbe wa Baraza wamepongeza huku pia wakimpongeza Rais wa Angola kwa kusaidia katika kujenga kuaminiana, kumaliza tofauti kati ya Rwanda na DRC,  kupitia mashauriano na hatimaye suluhu ya kudumu ya amani na usalama nchini DRC.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wanatambua hatua zinazochukuliwa kuweko kwa jeshi la kikanda la nchi za EAC na kupelekwa kwa vikosi vya Burundi na Uganda nchini DRC, na kusisitiza umuhimu wa ulinzi wa rai ana uratibu wa kazi hiyo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo Pamoja na pongezi hizo, wajumbe wametaka operesheni hizo za ulinzi zifanyike kwa kuzingatia sheria za kimataifa ikiwemo ya haki za binadamu na ile ya kiutu.

Tunatambua uhuru na mipaka ya DRC

Wajumbe wametambua pia uhuru na mipaka ya DRC na kuelezea utayari wao wa kutathmini Zaidi hatua zilizomo kwenye azimio namba 2641 la mwaka 2022, ikiwemo kuboresha, kusitisha au kuondoa vikwazo kadri itakavyoonekana inafaa kwa kuzingatia uzingatiaji wa azimio hilo.

Halikadhalika wamesisitiza  uungaji wao thabiti wa hatua za MONUSCO za kutekeleza majukumu yake ikiwemo ulinzi wa raia na kusihi kuendelea kwa juhudi hizo.

Bofya hapa kufahamu maazimio ya Baraza la Usalama la UN kuhusu vikwazo vya silaha DRC