Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani watoto milioni 4 nchini Pakistani bado wanaishi kwenye maji machafu yaliyotwama- UNICEF

Watu milioni 33 nchini Pakistani waliathiriwa na mafuriko makubwa yaliyokumba taifa hilo mwezi Septemba mwaka 2022
© WFP

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Pakistani, janga la uhai wa mtoto bado ni changamoto kubwa kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko zaidi ya miezi minne iliyopita huku idadi ya maambukizi  ya magonjwa ya hewa na utapiamlo uliokithiri au unyafuzi ikiendelea kuongezeka, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF wakati huu ambapo jumuiya ya kimataifa inajiandaa kwa ajili ya mkutano wa kuchangia taifa hilo la Asia ili lijenge mnepo dhidi ya majanga.

Tarehe 3 Novemba 2022 kijiji cha Jacobabad, jimboni Sindh nchini Pakistani, Surga mwenye umri wa miaka 15 akiteka maji kisima kinachotumia pampu. Nyumba yao ilisambaratishwa kwa mafuriko.
UNICEF/UN0730547/Bashir
Tarehe 3 Novemba 2022 kijiji cha Jacobabad, jimboni Sindh nchini Pakistani, Surga mwenye umri wa miaka 15 akiteka maji kisima kinachotumia pampu. Nyumba yao ilisambaratishwa kwa mafuriko.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Islamabad nchini Pakistani imesema zaidi ya miezi minne tangu kutangazwa kwa hali ya dharura, zaidi ya watoto milioni 4 bado wanaishi karibu au kwenye maji ya mafuriko  yaliyotwama na hivyo kutishia uhai na ustawi wao.

Hali ya afya ya watoto iko mashakani

Maambukizi makali kwenye njia ya hewa, moja ya sababu za vifo kwa watoto duniani, yameongezeka kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.

Halikadhalika, idadi ya watoto wenye unyafuzi kwenye maeneo yanayofuatiliwa na UNICEF imeongezeka maradufu kati ya Julai na Desemba ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka juzi wa 2021.

Takribani watoto milioni 1.5 wanahitaji lishe ya kukabiliana na unyafuzi ili kuokoa maisha yao.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Pakistan, Abdullah Fadil amesema watoto wanaoishi kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko wametumbukia zaidi kwenye majanga akisema, “mvua imekoma lakini janga la watoto bado limechachamaa. Takribani watoto milioni 10 wa kike na wa kiume bado wanahitaji misaada ya haraka ya kuokoa maisha na wanaingia msimu wa baridi kali bila malazi. Unyafuzi, magonjwa ya njia ya hewa, magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya maji yanaweka hatarini zaidi maisha ya watoto.”

Tarehe 3 Novemba 2022 kijiji cha Jacobabad, jimboni Sindh nchini Pakistani,  Surga mwenye umri wa miaka 15 ambaye nyumba yao ilisambaratishwa kwa mafuriko akiwa amembeba mdogo  wake Fayaz kwenye makazi ya muda.
UNICEF/UN0730552/Bashir
Tarehe 3 Novemba 2022 kijiji cha Jacobabad, jimboni Sindh nchini Pakistani, Surga mwenye umri wa miaka 15 ambaye nyumba yao ilisambaratishwa kwa mafuriko akiwa amembeba mdogo wake Fayaz kwenye makazi ya muda.

Viwango vya joto vimeshuka, wananchi hawana vikinga joto

Huko Jacobabad, wilaya ya kusini mwa Paksitani ambako familia hazina zaidi ya kitambaa kufunika makazi yao yaliyotwama kwenye maji, viwango vya joto nyakati za usiku vinashuka hadi nyuzijoto 7 katika kipimo cha Selsiyasi.

Katika maeneo ya milimani na nyanda za juu ambako nako mafuriko yamesababisha madhara, theluji imeanguka na viwango vya joto navyo ni chini ya nyuzijoto 0 katika kipimdo cha Selsiyasi.

UNICEF na wadau wanaendelea kutoa huduma za kuokoa maisha

Tayari UNICEF na wadau wameanza kusambaza vifaa kama nguo za kutia joto, blanketi wakilenga watu 200,000 wakiwemo watoto, wanawake na wanaume.

Kwa upande wa lishe, zaidi ya watoto 800,000 wamechunguzwa utapiamlo ambapo kati yao hao, 60,000 wamebainika kuwa na unyafuzi ambao ni pale mtoto anakuwa ni mwembamba kupindukia ukilinganisha na urefu wake na hivyo kupatiwa lishe maalum.

Huduma hiyo ya lishe imefikia takribani watu milioni 1.5 kupitia huduma za afya ya msingi.

Halikadhalika watoto milioni 4.5 wamepatiwa chanjo dhidi ya Polio katika wilaya 16 zilizokumbwa na mafuriko.

UNICEF na wadau pia wamepatia zaidi ya watu milioni 1 huduma za maji safi na salama, bila kusahau vikasha vya kujisafi kwa watu milioni moja.

Jimboni Sindh, Mkuu wa ofisi za UNICEF  mashinani nchini Pakistani Prem Chand akishuhudia jinsi mtoto Rahman mwenye umri wa miaka 11 akifurahi baada ya kuvaa koti wakati wa mgao wa vifaa vya kutia joto wakati wa baridi kali jimboni humo.
UNICEF/Arsalan Butt

Utoaji msaada unaenda sambamba na urejeshaji huduma

Pamoja na kutoa huduma hizo UNICEF inaendelea kurejesha huduma muhimu za afya, kujisafi na elimu kwenye maeneo yaliyoathirika ili wanaorejea makwao waweze kuendelea na maisha.

“Kadri familia zinavyorejea nyumbani, huduma zetu nazo zinaambatana nao,” amesema Bwana Fadil akiongeza kuwa huduma za afya, lishe na maji zinaendelea kufuata wananchi waliko.

Jamii ya kimataifa ‘fungueni pochi zenu’

Hata hivyo UNICEF inasema ili iweze kukamilisha operesheni zake kwa ufanisi, jamii ya kimataifa iongeze usaidizi wake kwa kutoa fedha kwa wakati.

“Kadri dunia inavyotazamia kusaidia kujikwamua na kujijenga upya kwa Pakistan, UNICEF inasihi nchi zipatie kipaumbele mahitaji ya sasa na ya  muda mrefu ya watoto kwa kutoa misaada ya kimkakati na endelevu,” imesema taarifa hiyo.

Ombi la sasa la UNICEF kufanikisha operesheni zake za kusaidia wanawake na watoto walioathiriwa na mafuriko Pakistani ni dola milioni 173.5 lakini limefadhiliwa kwa asilimia 37 pekee.

Familia za waliofurushwa makwao kutokana na mafuriko zikipatiwa msaada wa tibalishe ili kuepusha utapiamlo nchini Pakistani
© WFP/Marco Frattini
Familia za waliofurushwa makwao kutokana na mafuriko zikipatiwa msaada wa tibalishe ili kuepusha utapiamlo nchini Pakistani