Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyoka na N’ge watishia usalama wa wakimbizi kutoka Afghanistan na Pakistani nchini Sri Lanka

Wakimbizi kutoka Pakistani na Afghanistani walioko Sri Lanka wakiwa kwenye mahema yasiyo ya kudumu na mapagala baada ya kukimbia makazi yao kwa hofu ya kipigo na manyanyaso kufuatia msururu wa mashambulizi nchini Sri Lanka mwezi Aprili mwaka huu ambapo wa
UNHCR Video
Wakimbizi kutoka Pakistani na Afghanistani walioko Sri Lanka wakiwa kwenye mahema yasiyo ya kudumu na mapagala baada ya kukimbia makazi yao kwa hofu ya kipigo na manyanyaso kufuatia msururu wa mashambulizi nchini Sri Lanka mwezi Aprili mwaka huu ambapo watu 250 waliuawa.

Nyoka na N’ge watishia usalama wa wakimbizi kutoka Afghanistan na Pakistani nchini Sri Lanka

Msaada wa Kibinadamu

Ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu kufanyika kwa mashambulizi nchini Sri Lanka yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 250, takribani maelfu ya wasaka hifadhi, wahamiaji na wakimbizi wengi wao kutoka Pakistan na Afghanistan, bado wamesaka hifadhi mbali na nyumba zao kwa hofu ya vipigo na manyanyaso. John Kibego na taarifa kamili.

Ni kwenye mji wa Pasyala, ulioko nje kidogo ya mji mkuu wa Sri Lanka, Colombi, wakimbizi, wahamiaji na wasaka hifadhi kutoka Afghanistan na Pakistan wamehifadhiwa katika kituo cha ustawi wa jamii cha Amaddiya.

Idadi yao hapa ni takribani 600, wanawake, wanaume na watoto, mazingira yakiwa si salama na rafiki.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, wakimbizi wengine waliokimbia makazi yao baada ya msururu wa mashambulizi kwa hofu ya kushambuliwa  na kupigwa, wamesaka hifadhi misikitini na vituo vya polisi.

Hapa kituoni Amaddiya, UNHCR na wadau wanawapatia chakula, dawa na huduma nyingine muhimu, ikiwemo maji ambayo huletwa kwa lori kila siku. Waqas, mmoja wa wakimbizi anasimulia hali ilivyo..

“Tatizo si moja: Mvua ni tatizo, hakuna pahala pa kutosha kulala, hakuna chakula. Wanyama nao tatizo; kuna nyoka wakubwa, n’ge, ni hatari sana. Kila siku tunaua nyoka na n’ge. Hili si eneo zuri, tunataka kuhamia pahala pengine salama. Haya si maisha mazuri, hali ngumu sana.”

Nafasi finyu, ina maana wanaume lazima walale nje kwenye viambaza na mapagala na katika jengo kuu, zaidi ya wanawake na watoto 300 wanaishi kwenye vyumba vikubwa viwili vilivyo wazi, ikimaanisha hakuna faragha.

Hata hivyo shule chache na wahisani wamepatia watoto vitabu vya kuchora, penseli na wanasesere ili angalau watoto wawe na kitu cha kufanya. Fariha miongoni mwa wakimbizi anafunguka..

“Tunapata msaada, chakula na maji lakini tuna msongo wa akili hususan mazingira ya hapa ni magumu kwa watoto. Watoto wanapata matatizo mengi ya kiafya na usafi. Hatuna kabisa utulivu wa kifikra hapa.”

Hivi sasa UNHCR inashirikiana na mamlaka za Sri Lanka kujaribu kupata eneo mbadala salama ili kuhamishia familia hizo.