Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la kusaidia Pakistani laongezwa hadi dola milioni 816 kuepusha wimbi la pili la uharibifu

Maeneo ya makazi yaliyofurika kwenye kijiji kimoja jimboni Sindh nchini Pakistan.
© UNICEF/Asad Zaidi
Maeneo ya makazi yaliyofurika kwenye kijiji kimoja jimboni Sindh nchini Pakistan.

Ombi la kusaidia Pakistani laongezwa hadi dola milioni 816 kuepusha wimbi la pili la uharibifu

Msaada wa Kibinadamu

Wakati Pakistani ikihaha na kile kinachoitwa wimbi la pili la vifo na uharibifu kutokana na mafuriko makubwa yaliyokumba nchi hiyo mwezi Juni na kusababisha theluthi moja ya ardhi  ya taifa hilo kutwama, Umoja wa Mataifa umeongeza kiwango cha ombi la usaidizi wa kibinadamu kwa Pakistani kutoka dola milioni 160 hadi dola milioni 816.

Julien Harneis,  ambaye ni Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu, Pakistan amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa hali itazidi kuwa mbaya Pakistani iwapo misaada haifatikiwa. Hali kama vile ongezeko la vifo vya watoto, mlipuko wa magonjwa kama vile Malaria, homa ya Denge, ongezeko la utapiamlo.

Amesema serikali inahitaji msaada ili kuimarisha huduma za afya, lishe, maji na kujisafi katika maeneo yote ya nchi.

Mafuriko yameathiri watu milioni 33 nchini Pakistani, na imeripotiwa kuwa vifo ni takribani wanu 1,700 huku watu wengine milioni 20.6 wakihitaji misaada, imesema ripoti mpya ya hatua kwa mafuriko iliyochapishwa leo na Umoja wa Mataifa.

Takribani watu milioni 9.5 wanalengwa kupatiwa misaada ya kibinadamu hadi mwishoni mwa mwezi Mei mwakani.

Takribani wilaya 84 nchini kote zimekubwa na janga, zinaonesha takwimu za serikali, hasa hasa Balochistan, Sindh, na Khyber Pakhtunkhwa. Watu milioni 7.9 wamefurushwa makwao, huku takribani 600,000 wanaishi kwenye kambi za misaada. Yakadiriwa kuna wakimbizi 800,000 wakiwemo watoto 400,000.

“Tunahitaji hizi fedha, na tunahitaji haraka,” amesema Bwana Harneis akiongeza kuwa mkutano wa kimataifa wa kusaidia Pakistani utaitishwa baadaye mwaka huu ili kupata fedha zaidi za ujenzi mpya na ukarabati.

‘Kuna tishio la janga ya afya ya umma’ : Tedros

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika Geneva, Uswisi amesema takribani asilimia 10 ya vituo vya afya vimeharibiwa na mafuriko.

“Vifo vya watu zaidi ya 1,500 ni janga – hata hivyo ni ajabu kuwa watu wengi hawakupoteza maidha,” akiongeza kuwa hiyo ni kutokana na mipango na hatua za kipekee cha maonyo ya mapema na zilizofuatia za kuokoa zilizofanywa na serikali na jamii.

Serikali  ya Pakistan, amesema Dkt. Tedros, imezidiwa na inahitaji msaada wetu.

“Maji yaliacha kujaa lakini hatari haijaisha. Tuko kwenye hatari ya kupata janga la afya ya umma.”

Amesema zaidi ya wanawake 2,000 walio kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko wanajifungua kila siku na wengi wao katika mazingira yasiyo salama.

Msisitizo wa usaidizi kwa watu

“Vifo zaidi vinaweza kutokea kuliko hata vile vilivyosababishwa na mafuriko iwapo hatutahamasisha msaada mkubwa kwa Pakistan,” amesema Dkt. Tedros akitoa wito kwa hatua za pamoja kutoka kwa jamii ya kimataifa ambazo zitaangazia zaidi mahitaji ya watu badala ya mahitaji ya kila shirika.

Amesema ni muhimu kukumba kuwa bila kushughulikia kitisho kiletwacho na mabadiliko ya tabianchi, “tutakuwa tunachukua hatua kwenye dharura kama hizi na wakati mwingine mbaya zaidi.”