Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Tanzania kwa kuondoa marufuku ya mikutano ya hadhara

Mtaa moja jijini Dar es Salaam, bandari kubwa na ya kibiashara katika pwani ya Bahari ya Hindi nchini Tanzania. (Maktaba)
World Bank/Hendri Lombard
Mtaa moja jijini Dar es Salaam, bandari kubwa na ya kibiashara katika pwani ya Bahari ya Hindi nchini Tanzania. (Maktaba)

Heko Tanzania kwa kuondoa marufuku ya mikutano ya hadhara

Haki za binadamu

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, OHCHR, hii leo imepongeza hatua ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kutangaza kuondoa marufuku kwa vyama vya siasa nchini humo kufanya mikutano ya hadhara. 

Kauli hiyo ya OHCHR imetolewa na msemaji wa ofisi hiyo kutoka Nairobi, Kenya Seif Magango. 

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Bwana Magango amesema, "hatua hii ambayo ameichukua Rais Samia Suluhu Hassan kutupilia mbali marufuku dhidi ya mikutano ya vyama vya siasa nchini Tanzania ni hatua nzuri na pia ushindi mkubwa kwa demokrasia na haki za binadamu. Ikiwemo haki ya watu kukusanyika kwa hali ya amani na pia kujieleza kama wanavyotaka." -   

Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza hatua hiyo juzi Jumanne jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili. 

Alieleza kuwa uamuzi wake huo unazingatia mambo makuu manne  ambayo ni maridhiano, mnepo, marekebisho na ujenzi mpya. 

Pamoja na tangazo hilo, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kuikosoa na kuishauri serikali kupitia mikutano hiyo ya hadhara kistaarabu na kwa mujibu wa sheria na kanuni za taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Marufuku ya vyama vya siasa kutofanya mikutano ya hadhara ilipitishwa na mtangulizi wake Hayati John Magufulu miaka sita iliyopita.