Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 kuendelea kuwa mjadala 2023- WHO

Muuguzi akimtakasa mikono mgeni aliyetembelea hospitali ya mjini Masaka, Uganda
© UNICEF/Kalungi Kab
Muuguzi akimtakasa mikono mgeni aliyetembelea hospitali ya mjini Masaka, Uganda

COVID-19 kuendelea kuwa mjadala 2023- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limesema ingawa idadi ya vifo kutokana na ugonjwa wa COVID-19 ilipungua kwa mwaka jana wa 2022, bado tishio kutokana na ugonjwa huo linaendelea kwa mwaka huu wa 2023 na ugonjwa huo utaendelea kuwa mjadala na hatua zaidi za kinga na kitabibu zinapaswa kuendelea kuchukuliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi katika mkutano wake wa kwanza kwa mwaka huu wa 2023. 

Bado COVID-19 inasambaa kwa kasi maeneo ya kaskazini 

Amesema mwaka huu ikiwa ni wa nne tangu COVID-19 kutangazwa tishio la afya kwa umma duniani, licha ya maendeleo katika upatikanaji wa chanjo, matibabu na usimamizi wa ugonjwa huo bado COVID-19 imejikita. 

“Bado kuna ukosefu wa uwiano katika kupima, kutibu na chanjo na ndipo COVID-19 inasalia kuwat tishio kwa afya, uchumi na jamii. Kila wiki takribani watu 10,000 wanakufa duniani kwa COVID-19, idadi ambayo ndio inatufikia. Idadi halisi inaweza kuwa kubwa,”amesema Dkt. Tedros. 

Amesema  hofu yao kubwa zaidi ni taswira ya ugonjwa huo kutokana na kasi ya maambukizi kwenye maeneo mengi duniani na mnyumbuliko wa lahaja za virusi. 

“Katika wiki za karibuni kumekuweko na ripoti za ongezeko la wagonjwa wanaolazwa kutokana na COVID-19, hospitali kuzidiwa uwezo hasa katika maeneo ya kaskazini mwa dunia ambako magonjwa ya njia ya hewa ikiwemo homa ya mafua yanasambaa,” amefafanua Mkuu huyo wa WHO. 

China nako idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutokana na COVID-19 inaongezeka na “tumeendelea kuisihi China itupatie kwa kasi kubwa takwimu sahihi kuhusu wanaolazwa na vifo.” 

Dkt. Tedros amesema takwimu sahihi ni muhimu kwa WHO kuweza kufanya kazi yake na hivyo amesihi kila nchi ifanye hivyo. 

Hakuna maambukizi mapya ya Ebola Uganda tangu Novemba 2022 

Amezungumzia pia Ebola nchini Uganda akisema hakujakuweko na ripoti zozote za kupatikana kwa mgonjwa mpya tangu tarehe 27 mwezi Novemba mwaka 2022 na iwapo hali hiyo itaendelea basi ifikapo tarehe 11 mwezi huu wa Januari 2023, mlipuko wa Ebola nchini Uganda utatangazwa kuwa umemalizika.