Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda yatangaza kutokomezwa kwa mlipuko wa Ebola

Uchunguzi wa virusi vya Ebola kwenye mpaka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , DRC na Uganda
WHO/Matt Taylor
Uchunguzi wa virusi vya Ebola kwenye mpaka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , DRC na Uganda

Uganda yatangaza kutokomezwa kwa mlipuko wa Ebola

Afya

Uganda hii leo imetangaza kutokomeza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliosababishwa na virusi aina ya Sudan, ikiwa ni chini ya miezi minne tangu kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza kwenye wilaya ya Mubende nchini humo 20 mwezi Septemba mwaka jana. Taarifa ya Thelma Mwadzaya inafafanua zaidi. 

 

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO katika miji ya Brazaville, Congo na Kampala, Uganda imemnukuu Waziri wa afya wa Uganda Dkt. Jane Ruth Aceng Acero akisema wameweza kutokomeza ugonjwa huo haraka kutokana na kutekeleza kwa kasi mikakati muhimu ya udhibiti, usimamizi, ufuatiliaji wa wagonjwa na waambata wao sambamba na hatua za kinga na udhibiti wa maambukizi. 

Dkt. Acero amesema “pamoja na kupanua wito wa juhudi zetu na kuimarisha hatua zetu kwenye wilaya tisa zilizokuwa zimeathiriwa na Ebola, siri kuu ya mafanikio ni uelewa wa jamii zetu kuhusu umuhimu wa kile kilichopaswa kufanyika ili kutokomeza Ebola.” 

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Uganda kuwa na mlipuko wa Ebola ya virusi vya Sudan katika muongo mzima, ingawa ni mlipuko wa tano kwa ujumla wa ugonjwa wa Ebola. 

Taarifa hiyo imesema kulikuwa na wagonjwa 164 ambapo 142 walithibitishwa na 22 ni washukiwa.  

Kati yao hao, wagonjwa waliothibitishwa kufa kwa Ebola ni 55 ilhali 87 walipona. 

Zaidi ya watu 4000 ambao walikuwa waambata wa wagonjwa hao walifuatiliwa na afya yao kufuatiliwa kwa karibu kwa siku 21. 

Mgonjwa wa mwisho aliruhusiwa kutoka hospitali tarehe 30 mwezi Novemba mwaka jana ambapo siku 42 za kuhesabu ili kuona hakuna tena mgonjwa zilianza na hadi leo hakuna mgonjwa mpya wa Ebola. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesu amepongeza Uganda kwa hatua za kina ambazo zimefanikisha Ushindi wa leo wa kutokomeza Ebola. 

Amesema hatua ya leo inadhihirisha kuwa Ebola inaweza kutokomezwa pindi mfumo mzima unapofanya kazi pamoja,kuanzia kuwa na mfumo wa kutoa tahadhari, hadi kusaka na kuhudumia walioambukizwa pamoja na waambata wao bila kusahau kupata ushirikiano kutoka kwa jamii zilizoathirika. 

Dkt. Tedros amesema mafundisho kutokana nah atua za mlipuko huu uliotokomezwa na mifumo iliyowezesha kutokomeza ugonjwa huo utalinda waganda na wengineo katika miaka ijayo.