Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS na wadau wa kimataifa wahofia kuendelea kwa vurugu Greater Pibor na Jonglei

Mapigano ya kikabila katika eneo la Jonglei nchini Sudan Kusini yamesababisha utekaji nyara na mauaji. (Maktaba))
UNMISS
Mapigano ya kikabila katika eneo la Jonglei nchini Sudan Kusini yamesababisha utekaji nyara na mauaji. (Maktaba))

UNMISS na wadau wa kimataifa wahofia kuendelea kwa vurugu Greater Pibor na Jonglei

Amani na Usalama

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS, mpango wa Muungano wa Afrika Sudan Kusini AUMISS, IGAD, Troika, Muungano wa Ulaya EU na R-JMEC wamesema wana wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa ghasia, kupoteza maisha na ripoti za madai ya matumizi ya silaha nzito katika Eneo la Utawala la Greater Pibor na vijana wenye silaha kutoka jimbo la Jonglei. 

Washirika hao wanazitaka pande zote zinazohusika  katika machafuko kusitisha mara moja uhasama, kujizuia na kuheshimu haki za binadamu. 

Kwa mujibu wa taarifa ya UNMISS, AUMISS, IGAD, Troika, EU na R-JMEC iliyotolewa mjini Juba Sudan Kusini wanatoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini kuingilia kati kwa haraka ili kusitisha mapigano na kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na upatikanaji usiozuiliwa wa msaada wa kibinadamu kwa watu walioathiriwa na mapigano.  

Wanawake wa eneo la Greater Jonglei wakiwa katika barabara mpya iliyokarabatiwa mjini Pibor, Sudan Kusini.
UNMISS/Amanda Voisard
Wanawake wa eneo la Greater Jonglei wakiwa katika barabara mpya iliyokarabatiwa mjini Pibor, Sudan Kusini.

Pia wanasisitiza haja ya kuwachunguza na kuwawajibisha wahusika wote wa migogoro hiyo, wakiwemo wanaochocheavita na kuchochea ukatili na waliohusika na utekaji nyara wa wanawake na watoto. 

UNMISS na washirika hao wa kimataifa wanawahimiza sana wanasiasa wa kitaifa na viongozi wa kimila kuwashawishi vijana kuacha mara moja ghasia na kufuata njia ya mazungumzo inayozingatia kurejesha utulivu na kutatua kwa amani vyanzo vya mzozo. 

Wakati jukumu la msingi la kulinda raia ni la serikali ya mpito ya Sudan Kusini, UNMISS na washirika wa kimataifa wamesema “wako tayari kutoa msaada wote unaohitajika kulinda raia katika maeneo yaliyoathirika.” 

UNMISS inaimarisha doria katika maeneo yenye mizozo na kufuatilia kwa karibu hali ilivyo, ikibaini kwamba mapigano hayo katika siku za nyuma yamesababisha hasara kubwa ya maisha na raia wengi kufungasha virago na kukimbia. 

UNMISS, AUMISS, IGAD, Troika, EU na R-JMEC “wanasisitiza wito wa kusitishwa mara moja kwa ghasia hizi zisizotarajiwa ambazo zinahatarisha sana amani na utulivu wa watu wa Sudan Kusini.”  

Aidha wanaomba CTSAMVM kuchunguza ghasia na kuwataka wahusika wa pande zote katika mzozo huo kuwezesha ufikiaji wa watu wanaohitaji msaada. 

Mapigano ya kikabilia yameathiri jamii Pibor mashariki mwa Sudan Kusini.
UN Photo/Isaac Billy
Mapigano ya kikabilia yameathiri jamii Pibor mashariki mwa Sudan Kusini.

Watu 30,000 watawanywa na mapigano 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA limesema takriban watu 30,000 wametawanywa kufuatia mapigano ya hivi karibuni ya watu wenye silaha kwenye eneo la greater Pibor.

Sara Beysolow Nyanti, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini amesema “machafuko hayo yamesababishwa wizi wa ng’ombe, uharibifu wa vitu, na maelfu ya watu kutawanywa wakiwemio wakimbizi wa ndani 5000 wanaojumuisha wanawake na watoto waliowasili Pibor baada ya kukimbia vita Gumuruk na Lekuangole.” 

Ameongeza kuwa “Watu wametesema kiasi cha kutosha, raia hasa walio hatarini kama wanawake ,watoto, wazee na watu wenye ulemavu ndio wanaobeba gharama kubwa ya mgogoro huu unaoendelea.” 

Ametoa wito wa kusitishwa uhasama mara moja na kutoa fursa za ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa wenye uhitaji.