Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake kwenye sekta ya Afya wanalipwa 24% pungufu ya wenzao wa kiume

Muuguzi akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 katika kijiji cha Kasungu nchini Malawi
© UNICEF/Thoko Chikondi
Muuguzi akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 katika kijiji cha Kasungu nchini Malawi

Wanawake kwenye sekta ya Afya wanalipwa 24% pungufu ya wenzao wa kiume

Wanawake

Wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya afya na huduma wanalipwa ujira mdogo zaidi kuliko sekta nyingine za kiuchumi na wanalipwa asilimia 24 pungufu ya wenzao wa kiume hata pale wanapokuwa na vigezo sawa katika soko la ajira. 

Hayo yamebainishwa kwenye ripoti ya “Uchambuzi wa kina zaidi duniani kuhusu ukosefu wa usawa wa kijinsia kwenye mishahara katika sekta ya afya” uliofanywa na mashirika mawili ya umoja wa Mataifa lile la ajira duniani ILO na afya WHO na kusomwa jijini New York Marekani katika mkutano wa ngazi za juu unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. 

Ripoti huyo imefafanua kuwa pengo ghafi kati ya wanawake na wanaume ni takriban asilimia ishirini lakini likiangaziwa kwa undani zaidi kwenye masuala kama elimu, umri na muda wa kufanya kazi pengo hilo linaongezeka na kufikia asilimia 24 hii ikimaanisha kuwa wanawake wanalipwa kiwango cha chini zaidi kwenye soko la ajira ikilinganishwa na wanaume. 

Wanawake wanashikilia asilimia 67 ya nguvu kazi katika sekta ya afya.

Mtaalamu wa kuzuia na kudhibiti maambukizi wa WHO akiwashauri wauguzi katika kituo cha afya katika kambi ya Kutupalong jinsi ya kutoa huduma salama kwa wagonjwa wa COVID-19 bila kuambukizwa virusi.
WHO/Blink Media/Fabeha Monir
Mtaalamu wa kuzuia na kudhibiti maambukizi wa WHO akiwashauri wauguzi katika kituo cha afya katika kambi ya Kutupalong jinsi ya kutoa huduma salama kwa wagonjwa wa COVID-19 bila kuambukizwa virusi.

Ripoti hiyo imeenda mbali zaidi na kueleza kugundua kiujumla mishahara katika sekta ya afya ipo chini ikilinganishwa na sekta nyingine za kiuchumi na hii inaenda sambamba na ukweli kwamba sekta za kiuchumi ambazo wanawake ndio wengi nyingi zinakuwa na mishahara ya chini. 

Mkurugenzi wa kitengo cha nguvu kazi wa WHO Jim Campbell amesema “Ushahidi na uchambuzi uliomo kwenye ripoti hii lazima utumike kuzijulisha serikali, waajiri na wafanyabiashara kuwa wanatakiwa kuchukua hatua Madhubuti na pia kutumia habari njema za mafanikio katika nchi nyingine zilizoongeza mishahara na kuwa na utashi wa kisiasa katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye malipo.”

Zilipotafutwa sabababu zinazofanya wanawake kulipwa kidogo kuliko wanaume walio na sifa sawa za soko la ajira katika sekta ya afya na huduma kote ulimwenguni kwa kiasi kikubwa ripoti hiyo hiyo imesema sababu hazijaelezwa. 

Mkurugenzi wa Idara ya masharti ya kazi na usawa wa ILO Manuel Tomei amesema anatumai ripoti hii itasaidia kuchochea mazungumzo na hatua zinazohitajika kuleta usawa “Hakutakuwa na ahueni jumuishi, dhabiti na endelevu bila sekta ya afya na huduma imara. Hatuwezi kuwa na huduma bora za afya na uangalizi bila mazingira bora na ya haki ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na mishahara ya haki kwa wafanyakazi wa afya na huduma, ambao wengi wao ni wanawake. Wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti za kisera ikijumuisha mazungumzo muhimu ya kisera kati ya taasisi.”

Ripoti hiyo imekumbusha namna janga la COVID-19 lilivyoionesha dunia umuhimu wa sekta hiyo na wafanyakazi wake na kueleza kuwa sekta ya afya na huduma imestahimili malipo duni kwa ujumla na mapungufu makubwa ya mishahara ya kijinsia na mazingira magumu kwa kipindi kirefu na kwamba ni wakati muafaka wafanyakazi hao waangaliwe upya na kufanyika kwa mabadiliko kuanzia kwenye sera za nchi.