Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM na EU kuwasaidia Waukraine 700,000 wakati huu wa msimu wa baridi

Huko Bucha, Ukraine, wakaazi wanajiandaa kukabiliana na majira ya baridi bila umeme.
OHCHR/Anthony Headley
Huko Bucha, Ukraine, wakaazi wanajiandaa kukabiliana na majira ya baridi bila umeme.

IOM na EU kuwasaidia Waukraine 700,000 wakati huu wa msimu wa baridi

Msaada wa Kibinadamu

Wakati huu ambapo msimu wa baridi kali ukishika kasi na kufikia nyuzi joto sifuri kote nchini Ukriane, Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM nchini Ukraine, imetangaza kuongeza msaada kwa wakimbizi wa ndani walioathirika na vita inayoendelea nchini humo ambao kwa sasa wanakabiliwa na baridi kali.

Taarifa ya IOM imeeleza kuwa kwa ufadhili wa fedha kutoka Muungano wa Ulaya EU wataweza kuwasaidia zaidi ya Waukraine 700,000 kwa usaidizi katika sekta mbalimbali wakati wote wa miezi ya baridi, ambayo itakuwa msimu wenye changamoto nyingi zaidi kwa nchi hiyo.

Msaada unaotolewa na IOm kwa msaada wa EU unajumuisha ukarabati wa vituo vya pamoja vya kuwahifadhi watu waliohamishwa makazi yao, uboreshaji wa usambazaji wa huduma za maji, udhibiti wa maji taka na mifumo ya kupasha joto, ukarabati wa nyumba zilizoharibiwa, pamoja na usambazaji wa mablanketi ya joto, vitanda, magodoro na vifaa vya usafi.  

Unajumuisha pia utoaji wa mafuta na usaidizi wa pesa taslim unaowawezesha watu kuwa na njia rahisi za kujikimu wakati wa majira ya baridi. 

Msichana wa miaka 8  akiwa nje ya nyumba yao katika kijiji cha Uhryniv Ukraine
© UNICEF/Yana Sidash
Msichana wa miaka 8 akiwa nje ya nyumba yao katika kijiji cha Uhryniv Ukraine

Ukarabati utakaofanywa 

IOM inasema, timu zake zinazotembea kila Konda nchini humo zitafanya kazi za ukarabati katika maeneo na taasisi za kijamii 375 kuboresha mifumo ya upashaji joto, kurekebisha paa zinazovuja, kubadilisha madirisha yaliyovunjika, kuweka via vya kupasha joto nyumba na kutoa zisizofanya kazi, na kufunga mabomba ya  ziada ya kuogea.  

IOM pia itakarabati nyumba 5,800 za watu binafsi na kusambaza vifaa vya dharura ili kuwawezesha watu kufanya ukarabati wao wenyewe.  

Mafuta pia yatatolewa ili kusaidia familia kuwa na joto wakati wa baridi. Zaidi ya hayo IOM pia itasaidia manispaa katika maeneo yaliyochukuliwa tena na Serikali ya Ukraine hivi majuzi yenye vifaa vya ujenzi na jenereta. 

Anh Nguyen, mwakilishi wa IOM Ukraine amesema "Watu waliokimbia makazi yao na walioathiriwa na vita watakabiliwa na changamoto mpya na zinazoongezeka huku vita vikiendelea na msimu wa baridi kali kuikumba Ukraine. Kipaumbele chetu kikuu ni kuunga mkono usaidizi wa kuwapa vipashajoto salama, na vyenye heshima ili kuwasaidia watu kustahimili miezi michache ijayo.”  

Naye Claudia Amaral, mkuu wa misaada ya kibinadamu wa EU nchini Ukraine amesema "Watu walio katika mazingira magumu nchini Ukraine wanapitia majira ya baridi kali zaidi. Huku mashambulizi yakiendelea na kuacha mamilioni bila upatikanaji wa umeme, joto na maji, washirika wetu wa kibinadamu kama IOM wanaendelea kufanya kazi ili kukidhi mahitaji muhimu zaidi,"  

IOM ikijaribu kufanya ukarabati Ukraine kuwasaidia watu waliotawanywa na vita kukabiliana na baridi kali
IOM / Iryna Tymchyshyn
IOM ikijaribu kufanya ukarabati Ukraine kuwasaidia watu waliotawanywa na vita kukabiliana na baridi kali

Asilimia 40 ya watu wanahitaji msaada 

Takriban Waukraine milioni 18, au asilimia 40 ya wakazi wa nchi hiyo, wanahitaji msaada wa kibinadamu, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya Kibinadamu OCHA.  

Imeongeza kuwa mashambulizi yanayoendelea dhidi ya miundombinu muhimu ya Ukraine yamezidisha athari mbaya za vita na hatari kwa watu walioathiriwa zaidi. 

Utafiti wa hivi karibuni wa IOM unaonyesha kuwa licha ya mashambulizi mengi kwenye miundombinu ya usambazaji wa umeme na joto nchini, wananchi wa Ukraine wanapanga kusalia majira haya ya baridi katika maeneo yao ya sasa ni asilimia saba tu ya waliohojiwa kote nchini, wengine wanafikiria kuondoka. Wakati huo huo, rasilimali binafsi kwa ajili ya maisha zinazidi kuwa chache, kwani asilimia 43 ya familia zote nchini Ukraine zimemaliza kabisa akiba zao.