Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Ukraine wanawasili Poland katika "hali ya dhiki na wasiwasi"-UNHCR

Wakimbizi wa Ukraine waliowasili kituo cha treni cha Rzeszow nchini Poland.
© UNHCR/Maciej Moskwa
Wakimbizi wa Ukraine waliowasili kituo cha treni cha Rzeszow nchini Poland.

Wakimbizi wa Ukraine wanawasili Poland katika "hali ya dhiki na wasiwasi"-UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya wakimbizi wa Ukraine walio katika mazingira magumu wanaowasili Poland, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeongeza shughuli zake ili kutoa msaada huku Poland ikiendelea kuwa nchi  amabayo imepokea wakimbizi wengi kutoka Ukraine. 

Zaidi ya wakimbizi milioni 3.5 wameingia nchini tangu kuanza kwa vita tarehe 24 Februari. 

Akizungumza kutoka Warsaw katika mkutano na waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva,Uswisi  msemaji wa UNHCR Olga Sarrado amesema kwamba "wakimbizi wapya mara nyingi hutoka katika maeneo yaliyoathiriwa sana na mapigano, wengine wakiwa wamejificha kwa majuma kadhaa kwenye makazi ya mabomu na vyumba vya chini ya ardhi,"  

Ameongeza kwamba "Mara nyingi hufika wakiwa katika hali ya dhiki na wasiwasi, wakiwa wamewaacha wanafamilia nyuma, bila mpango wazi wa wapi pa kwenda, na rasilimali chache za kiuchumi na watu wanowafahamu kuliko wale waliokimbia mapema." 

Ametanabaisha kuwa "kasi ya kuwasili imepungua ikilinganishwa na mapema Machi, wakati zaidi ya watu 100,000 walikuwa wakifika kwa siku, hadi takriban watu 20,000 kila siku katika kipindi cha Mei", Olga Sarrado ameongeza kuwa "pia tumeona harakati zaidi za kuingia na kutoka , ambapo watu hutoka na kurudi kutoka Ukraine kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kuangalia mali zao, kutembelea familia, au kurudi kazini.” 

Huduma za afya na mahitaji ya matibabu ndiyo masuala makuu ambayo wafanyakazi wa UNHCR hupokea kutoka kwa wakimbizi. 

Maombi mengine yanahusu usafiri, usaidizi wa kifedha, mahitaji ya kisaikolojia na kijamii, malazi, na upatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu na wazee. 

UNHCR inakadiria kuwa takriban "asilimia 50 kati yao wangependa kusalia Poland". 

Kulingana na Olga Sarrado, “mamlaka nchini Poland pia walikuwa wametaja kwamba kati ya milioni 1.5 hadi 2 wangebaki katika nchi yao.” 

Kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani kutokana na uharibifu mkubwa na uhasama unaoendelea nchini Ukraine, Poland inatarajia kuendelea kupokea idadi kubwa ya wakimbizi. 

Poland imeweka mifumo ya kuhakikisha kukaa ndani ya sheria, kupata ajira, elimu, huduma za afya, na mipango mingine ya ustawi wa jamii kwa wakimbizi wa Ukraine. 

"Zaidi ya milioni 1.1 wamejiandikisha na mamlaka ya Poland, kumaanisha kuwa wamepokea nambari ya kitambulisho cha serikali (Inaitwa PESEL), ambayo inawapa fursa kwa ajili ya  ufikiaji wa huduma; Asilimia 94 ya waliosajiliwa ni wanawake na watoto”, amesema Sarrado. 

UNHCR ilianzisha mpango wake wa msaada wa pesa taslimu mwezi Machi. Aidha imeanzisha vituo vinane vya uandikishaji fedha katika maeneo makuu yanayohifadhi wakimbizi, ikiwa ni pamoja na Warsaw, Krakow, Poznan, Wroclaw, Ostroda, Gdynia, na Gdansk. 

Zaidi ya wakimbizi 100,000 kutoka Ukraine tayari wamepokea usaidizi wa kifedha kutoka UNHCR ili kugharamia mahitaji yao ya kimsingi, kama vile kulipa kodi au kununua chakula na dawa. 

Kwa mujibu wa UNHCR, "karibu asilimia 20 ya wakimbizi hao waliojiandikisha kupokea msaada wa pesa taslimu wana mahitaji maalum." 

Bi Sarrado ameongeza kwamba,"msaada hutolewa kwa watu walio na mahitaji ya kiafya ya dharura, wazee, akina mama wanao lea watoto wenyewe, wanawake walio katika hatari na watu wenye ulemavu, na nusu ya watoto wenye mahitaji maalum ambao wametenganishwa au waliosafiri bila kuandamana na mtu." 

Msaada wa Pesa hutolewa kwa miezi mitatu kwa wale wanaohitaji zaidi hadi waweze kujikimu vyema au kujumuishwa katika mifumo ya serikali ya hifadhi ya jamii.