Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2022 uliweka rehani afya za mamilioni ya watu duniani: WHO

Umoja wa Mataifa katika juhudi za kuzuia COVID-19 nchini Guinea-Bissau
UNIOGBIS
Umoja wa Mataifa katika juhudi za kuzuia COVID-19 nchini Guinea-Bissau

Mwaka 2022 uliweka rehani afya za mamilioni ya watu duniani: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limesema mwaka 2022 umegubikwa na changamoto lukuki za kiafya, kuanzia janga la COVID-19, Ebola, Mpoxy hadi vita vilivyokatili na kujeruhi wengi hata hivyo limeeleza kuona matumaini katika mwaka ujao, matumaini yapi?

Taarifa ya tathmini ya kiafya ulimwenguni iliyotolewa leo na WHO nchini Geneva Uswisi imeeleza mwaka 2022, umeendelea kushuhudia uwepo wa janga la COVID-19 pamoja na mlipuko wa ugonjwa wa Mpox hapo awali ikifahamika kama Monkeypox ambao ulienea kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani.

Katika pembe ya Afrika na Ukanda wa Sahel nchi nyingi zimekabiliwa na milipuko ya kipindupindu, utapiamlo na magonjwa mengine nyemelezi kutokana na ukame

Wananchi wa Ethiopia na Ukraine wamekabiliwa na kifo na uharibifu unaoletwa na vita. Ebola ilipiga hodi nchini Uganda, na mafuriko makubwa nchini Pakistan yameweka mzigo mkubwa kwenye sekta ya afya yan chi hiyo.

Bila kutaja matishio mengine mengi kwa afya ambayo watu hukabiliana nayo mwaka hadi mwaka, magonjwa yatokanayo na mazingira, bidhaa wanazotumia, maeneo wanayoishi na kufanya kazi, na ukosefu wao wa ufikiaji wa huduma muhimu za afya.

Hata hivyo Pamoja na changamoto zote hizi, mwaka unamalizika kwa matumaini, kwani wagonjwa wa COVID-19 na Mpox wameendelea kupungua, huku kukiwa hakuna mgonjwa hata mmoja wa Ebola kuripotiwa tangu tarehe 27 mwezi uliopita wa Novemba.

WHO imeeeleza ina matumaini kwamba kila moja ya dharura hizi itatangazwa imemalizika mwaka ujao.

Hata hivyo ugonjwa wa malaria bado unatesa wananchi wengi duniani lakini kuna juhudi zinafanyika kila mahali kuhakikisha hakuna ongezeko Zaidi na ingawa idadi ya wagonjwa imeongezeka lakini kasi ya wagonjwa imepungua ikilinganisha na miaka uliyopita.

Juhudi nyingine zinazofanyw ana WHO ni Pamoja na kutoa ripoti za kina za kimataifa  na miongozo kwa serikali katika maeneo mbalimbali ikiwemo jinsi ya kubadilisha huduma za afya ya akili, kuongeza viwango vya mazoezi ya mwili, na kuzuia magonjwa ya kinywa ambayo yanaathiri karibu nusu ya idadi ya watu ulimwenguni.