Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante Umoja wa Mataifa kupitia uhamiaji sasa nina familia Tanzania- Oscar

Oscar Kalere Oscar, mhamiaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na anaaishi nchini Tanzania tangu mwaka 2002 na sasa anafanya kazi ya uchungaji.
UN News
Oscar Kalere Oscar, mhamiaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na anaaishi nchini Tanzania tangu mwaka 2002 na sasa anafanya kazi ya uchungaji.

Asante Umoja wa Mataifa kupitia uhamiaji sasa nina familia Tanzania- Oscar

Wahamiaji na Wakimbizi

Ikiwa ni siku chache zimepita tangu dunia kuadhimisha siku ya wahamiaji duniani, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la uhamiaji, IOM,  ukitoa wito kwa jamii ya kimataifa na nchi wanachama wa Umoja huo  kushiriki katika kufanikisha uhamiaji wa wale wanaokimbia ghasia makwao na halikadhalika wale wanaosaka fursa bora, mmoja wa wanufaika wa uhamiaji ametoa shukrani zake kwa taifa ambalo limempatia hifadhi baada ya kukimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Huyo si mwingine bali ni Oscar Kalere Oscar, ambaye sasa ni mhamiaji nchini Tanzania na katika mazungumzo na Idhaa ya Kiswahili ya  Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Oscar aliulizwa kulikoni anaishi Tanzania na yeye ni raia wa DRC akasema, “ni suala ambalo liko wazi unapozungumzia taifa la DRC au unapotaja DRC, moja kwa moja unapata picha ya nchi hiyo ambayo imekuwa katika vita kwa muda mrefu. Kwa hiyo unaposikia mkongomani yuko nchi Jirani inaleta picha kwamba ni kutafuta mahali ambapo penye  usalama au amani iliyoshiba, amani ambayo inajitosheleza ili uweze kukaa pia kwa usalama, na hicho ndio kilinifanya niondoke DRC na niwepo Tanzania.”

Milio ya risasi ilitufurumusha tukakimbia DRC na kuingia Tanzania

Oscar anasema mwaka huo wa 2002 ni vita iliibuka ikianzishwa na waasi wa RCD waliokuwa wanashikilia eneo la mashariki mwa DRC.  “Kwa hiyo kukawa hakuna amani kabisa. Nakumbuka siku kulikuwa na milio mingi ya risasi, kwa hiyo kila mtu alikuwa anatafuta namna ya kukimbia. Sasa mimi hali hii ilinikuta niko Uvira, karibu na Ziwa Tanganyika, na meli zilikuwa zimeshaondoka, basi tukapanda boti. Kwa neema ya Mungu tukafika Kigoma basi tukapanda treni.”

Anasema hakuwa peke yake safarini, bali alikuwa na wenzake wengine. Boti ilipita visiwa kama vile Baraka, Swima, Kazimia hadi Kigoma. “Na Kigoma tulikaa siku mbili tu kusubiri ratiba ya treni kisha tukakata tiketi tukaja Dar es salaam.”

Oscar Kalere Oscar ni mhamiaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye sasa anaishi nchini Tanzania.
UN News
Oscar Kalere Oscar ni mhamiaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye sasa anaishi nchini Tanzania.

Maisha baada ya kufika Dar es salaam- Kupata vibali vya uhamiaji

Baada ya kufika Dar es salaam, wakongomani wenzao waliokuwa wamefika Tanzania siku nyingi waliwapokea Oscar na wenzake. “Walitupokea na kutuonyesha mji kwa hiyo tukawa wenyeji tukauelewa mji, tukafuata utaratibu unaotakiwa kwa ajili ya kuishi kwa usalama. Tukapata vibali, hati za kusafiria na vibali vya kufanya kazi. Maisha yakaendelea hadi wengine tumeolea Tanzania, tuna familia Tanzania, na hata sasa tunachofanya Tanzania kama kazi, utumishi au huduma, tunafanyia Tanzania. Maisha ni mazuri. Unajua mahali penye amani lazima maendeleo yanakuwepo.”

Tweet URL

Sasa mimi ni mhamiaji na si mkimbizi na ana neno kwa Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi, wa mwaka 1951, mkimbizi anakoma kuwa mkimbizi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuambua kuanzisha maisha katika nchi ile aliyokimbilia.  Hatua hii ni ambayo Oscar ameifuata na hivyo kuanzisha maisha nchini Tanzania na sasa ana familia na shughuli anayofanya ni mchungaji.

“Mimi nashukuru Umoja wa Mataifa kwa hiyo será yake inayoweza kuruhusu wanachama wa chombo hicho kuweza kutekeleza kama mgeni anaingia katika nchi yako anaweza kupokelewa na baadaye anapewa fursa ya kuendelea au kujiendeleza kimaisha,” anasema Oscar.

Shukrani sana kwa Tanzania

Mhamiaji huyu hakuwa mnyimi wa shukrani kwa taifa la Tanzania lililompatia hifadhi akisema, “Tanzania ni nyumbani na nichukue fursa hii kwa niaba ya wakongo walioko Tanzania kuishukuru kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ukarimu wake kwa wageni. Tunafahamu wakimbizi wengu wako pake kutoka nchi jirani, si tu DRC. Nisema tu pia watanzania ni wakarimu.”