Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru ya amani iking’ara Ethiopia, UNHCR yataka majawabu ya kudumu ya usaidizi kwa wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Filippo Grandi akiwa ziarani Ziara ya wakimbizi wa Eritrea waliokimbia makazi yao kutokana na vita katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia
© UNHCR/Samuel Otieno
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Filippo Grandi akiwa ziarani Ziara ya wakimbizi wa Eritrea waliokimbia makazi yao kutokana na vita katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia

Nuru ya amani iking’ara Ethiopia, UNHCR yataka majawabu ya kudumu ya usaidizi kwa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Filippo Grandi, amehitimisha ziara yake ya siku tatu nchini Ethiopia na kusisitiza msimamo wake wa kuunga mkono hatua za kiutu kwa wakimbizi na wakimbizi wa ndani nchini Ethiopia, na kufanya kazi ili kupata majawabu ya muda mrefu ikiwemo wale waliofurushwa makwao kutokana na ukame na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. 

Taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR mjini Addis Ababa, Ethiopia imemnukuu Bwana Grandi akisema, “ingawa miaka michache ya hivi karibuni imekuwa migumu na michungu kwa wengi walioathiriwa na mzozo nchini Ethiopia, nimetiwa moyo kuona maendeleo yaliyofikiwa katika kusaka amani nchini Ethiopia na kuona juhudi zilizofanyika kupatia misaada watu waliopoteza kila kitu.” 

Hali ya usaidizi inatia moyo 

Wakati wa ziara hiyo alikuwa na mazungumzo na maafisa waandamizi wa serikali na jamii za wakimbizi wa ndani na wale wanaotoka nje ya nchi wakiwemo wakimbizi kutoka Eritrea. 

Tangu makubaliano ya amani ya mwezi Novemba mwaka jana, UNHCR na wadau wengine wamekuwa wakiimarisha hatua zao za kufikisha misaada muhimu kwa wakimbizi, zikiwemo dawa, vifaa vya kujenga makazi, nguo, vifaa vya majumbani na blanketi. 

“Maendeleo ni dhahiri hapa mashinani. Watu sasa wanapata miaada. Baadhi wamerejea nyumbani, lakini mahitaji zaidi yanasubiriwa ili kusaidia ujenzi mpya na jitihada za kujikwamua katika maeneo ya Afar, Amhara na Tigray,” amesema Bwana Grandi. 

Amesisitiza kuwa itakuwa muhimu sana kuimarisha mazingira ya maisha na kufanya kazi kuapta majawabu ya kudumu, ikiwemo watu kuweza kurejea kwa hiari kwenye makazi yao.

Familia moja kutoka Eritrea wakiwa nje ya makazi yao katika eneo la wakimbizi katika mkoa wa Amhara nchini Ethiopia.
© UNHCR/Samuel Otieno
Familia moja kutoka Eritrea wakiwa nje ya makazi yao katika eneo la wakimbizi katika mkoa wa Amhara nchini Ethiopia.

Msaada zaidi kwenye eneo wanaloishi wakimbizi kutoka Eritrea 

Ziara hiyo ilimfikisha pia kwa wakimbizi kutoka Eritrea waliohamishiwa eneo la Alemwach, takribani kilometa 70 kutoka mji wa Gondar jimboni Amhara na sasa ni makazi ya watu 22,000. 

Eneo hilo la Alemwach pamoja na kuwa na mazingira salama, bado linahitaji uwekezaji zaidi kuhakikisha wakimbizi wanaweza kujenga upya maisha yao. 

Halikdhalika, huduma za afya, elimu, kujisafi na usafi lazima ziimarishwe ili wakimbizi na wenyeji waweze kustawi kiafya na kielimu kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi, GCR. 

Mkataba huo unalenga kuimarisha mshikamano baina ya wakimbizi nan chi zinazowapokea, pamoja na kuwezesha wakimbizi kujitegemea na kupata suluhisho za kudumu. 

Ethiopia imekumbatia vema GCR 

“Mfumo huo wa GCR umepokewa vema na Ethiopia ambayo imeweka mazingira jumuishi kupitia mradi wa kusaidia wakimbizi na wenyeji na hiki kinapaswa kuigwa duniani kote na inatia moyo kuona juhudi za serikali za kufanikisha hatua hiyo hapa Ethiopia,” amesema Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR. 

Tweet URL

Viongozi aliokutana nao wakati wa ziara hiyo ni pamoja na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, Demeke Mekonnen na maafisa wengineo ambao amewashukuru kwa kuendeleza ukaribu wao kwa wakimbizi. 

Grandi amesema nchi nyingi zingaliamua kufunga milango yao wakati zikikumbwa na mzozo na mabadiliko ya tabianchi, “lakini serikali na watu wa Ethiopia mmeendelea na ukaribu wa kupokea na kuhifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini na Somalia.” 

Ametoa wito kwa usajili wa haraka wa wakimbizi wapya wanaowasili na amesihi jamii ya kimataifa iimarishe usaidizi wake wa kifedha na kuchagiza utoajiwa misaada muhimu ya kibinadamu. 

Mwaka 2022, miradi ya UNHCR nchini Ethiopia ilipata ufadhili kwa asilimia 50 pekee na kufanya iwe moja ya operesheni 12 za UNHCR zinazopokea kiwango kidogo zaidi cha fedha duniani. 

Kwa mwaka huu wa 2023, mahitaji zaidi yakiongezeka halikadhalika ukimbizi wa ndani utokanao na ukame, UNHCR inahitaji dola milioni 370 kusaidia, kulinda na kusaka majawabu kwa wakimbizi na familia zilizofurushwa makwao Ethiopia.