Ukarimu wa Rwanda wafanya mkimbizi asahau kama ni mkimbizi
Nchini Rwanda ukarimu na fursa wanazopata wakimbizi vimesababisha wakimbizi hao wajisikie nyumbani na hata kusahau kuwa wao wenyewe ni wakimbizi.
Miongoni mwa wakimbizi hao ni Ali Abdi, mkimbizi kutoka Somalia, ambaye alisaka hifadhi mjini Kigali, Rwanda miaka 20 iliyopita wakati nchi yake ilipokuwa imegubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Akiwa Rwanda, maisha awali yalikuwa magumu kwa kuzingatia hakufahamu lugha lakini ukimbizi haukumzuia kupata mpenzi wake wa maisha ambaye ni Jasmine Mukagashagaza.
“Mke wangu anatoka nchi hii, amenifundisha mengi na sasa ninaweza kuwa huru.”
Rwanda ni nchi ambayo inaruhusu wakimbizi kushiriki kwenye biashara na Ali ni mjasiriamali akiuza bidhaa ndogondogo.
“Wakati mwingine nasahau kama mimi ni mkimbizi. Nakumbuka tu pale ninapoona kadi yangu ya ukimbizi au watu wanaponiita mkimbizi.”
Ali ni shuhuda wa utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi ambapo anasema..
“Naishi kama raia yeyote wa nchi hii. Nazungumza lugha yao na marafiki zangu wa miaka 17 wanatoka nchi hii.”
Kwa sasa Ali na mkewe Jasmine wameweza kujenga nyumba yao wakiishi na watoto wao watano na ndoto ya Ali ni..
“Nataka wasome na wafanya kazi kwa bidi ili wasikumbane na matatizo kama niliyokumbana nayo mimi. Hiyo ndio ndoto yangu.”
Rwanda inahifadhi zaidi ya wakimbizi 150,000 ambapo 12,000 kati yao wanaishi kwenye miji kama vile Kigali.