Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je maisha ya wahamiaji hapo uliko wewe yako vipi? Tafakari chukua hatua- Guterres

Romeu Mauricio na mtoto wake wa umri wa miaka mitatu wakivuka eneo la Darien linalotenganisha Colombia na Panama
© UNICEF/William Urdaneta
Romeu Mauricio na mtoto wake wa umri wa miaka mitatu wakivuka eneo la Darien linalotenganisha Colombia na Panama

Je maisha ya wahamiaji hapo uliko wewe yako vipi? Tafakari chukua hatua- Guterres

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka maadhimisho ya leo ya siku ya wahamiaji duniani yatumike kutafakari maisha ya watu zaidi ya milioni 280 ambao wamelazimika kuondoka nchi zao kusaka fursa, utu, uhuru na maisha bora.

Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku hii ya wahamiaji duniani inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 18 mwezi desemba kufuatia azimio namba 55/93 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 4 mwezi desemba mwaka 2000.

Uhamiaji una pande mbili za tamu na chungu

Katibu Mkuu amesema leo hii, zaidi ya asilimia 80 ya wahamiaji duniani kote walivuka mipaka kwa kupitia njia salama na kufuata taratibu zinazotakiwa.

“Uhamiaji ni kichocheo thabiti cha ukuaji uchumi, mabadiliko ya mienendo ya kijamii na maelewano,” amesema Katibu Mkuu.

Hata hivyo amesema uhamiaji usiofuata kanuni unazidi  kushamiri na wahamiaji wanapitia njia za kutisha na za kikatili  wakikumbwa na wasafirishaji haramu katili wanaoendelea kunufaika kwa gharama yoyote.

Umoja wa Mataifa unasema katika kipindi cha zaidi ya miaka 8, takribani wahamiaji 51,000 wamekufa na maelfu zaidi wametoweka. “Nyuma ya kila hiyo namba ni binadamu- awe ni dada, kaka, mtoto wa kike, mtoto wa kiume, mama au mama,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu anasema Haki za Mhamiaji ni haki za binadamu. Lazima ziheshimiwe bila ubaguzi wowote ule – iwe anakimbia nchi yake kwa kulazimishwa, anaondoka kwa hiari, anaondoka rasmi kwa kuruhusiwa ama la.

Lazima hatua zichukuliwe kulinda wahamiaji

Guterres anasema  “lazima tuchukue hatua tunazoweza kuepusha kupotea kwa uhai – kama ilivyo misingi ya kiutu na wajibu wetu kimaadili na kisheria. Lazima tuweke mfumo wa kusaka na kuokoa halikadhalika matibabu kwa wahamiaji.”

Ametaka pia kupanuliwa kwa wigo wa mbinu za uhamiaji zinazojali haki za binadamu na pia kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kutatua suala la ukosefu wa nguvu kazi.

“Lazima pia tuweke usaidizi wa kimataifa kwenye uwekezaji kule wahamiaji wanatoka ili kuhakikisha uhamiaji ni mtu anaamua na si lazima aondoke,” amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kuwa hakuna janga la uhamiaji bali janga la mshikamano. “Leo kuliko wakati wowote ule hebu tulinde utu wetu wa pamoja na kurejesha haki na utu kwa kila mtu.”

Bofya hapa kupata ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM António Vitorino.