Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA Tanzania yakabidhi msaada wa dawati la jinsia wilayani Simanjiro

Jengo la dawati la jinsia na watoto kwa ajili ya kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia na mila kandamizi dhidi ya wanawake na wasichana
Picha: UNFPA/Warren Bright
Jengo la dawati la jinsia na watoto kwa ajili ya kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia na mila kandamizi dhidi ya wanawake na wasichana

UNFPA Tanzania yakabidhi msaada wa dawati la jinsia wilayani Simanjiro

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na masuala ya afya ya uzazi UNFPA nchini Tanzania limekabidhi jeshi la polisi mkoani Manyara msaada wa jengo la dawati la jinsia na watoto ikiwa njia moja wapo ya jitihada za kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia na mila kandamizi dhidi ya wanawake, wasichana na watoto.

Sherehe ya kukabidhi jengo hilo la jinsia ilipambwa na nyimbo kutoka kwaya ya Simajiro wakiimbia nyimbo za pongezi na shukrani kwa UNFPA Tanzania huku pia wakielezea changamoto ya ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto wa wilaya ya Simanjiro iliyoko mkoa wa Manyara Kaskazini mwa Tanzania.

Jengo hili ni moja kati ya majengo 10 yanayojengwana UNFPA nchini Tanzania na Msaidizi wa Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania Dkt. Majaliwa Marwa anaeleza kwanini wanajenga majengo haya.

“Tunaamini kwamba kupitia majengo haya tunatoa fursa kwa wananchi kuripoti Matukio ya ukatili na Matukio haya kufanyiwa uchunguzi na hatimaye wahusika kuchukuliwa hatua. Tunaamini pia kuwepo kwa madawati haya kunatoa hamasa ya jamii na wananchi kuripoti Matukio, kuzungumza kuhusu ukatili, lakini pia tunawawezesha jeshi la polisi kufanya kazi katika mazingira ambayo ni rafiki wakiwa na vitendea kazi na mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi.”

Katika Mkoa wa Manyara UNFPA wanajenga madawati matatu ambapo Kamishna Msaidizi wa Polisi George Katabazi ambaye pia ni kamanda wa polisi mkoa wa Manyara anasema itasaidia sana kukabiliana na changamoto wanazo kabiliana nazo .

“Haya madawati ya jinsia kwa mkoa wa Manyara ni njia mojawapo ya kupambana na ukatili wa kijinsia na watoto katika mkoa wa wetu. Haya Matukio ni changamoto katika mkoa wetu kwa maana kwamba watoto wanafanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, kulawitiwa lakini sio watoto pekeyao vilevile na wanawake, lakini watoto sana ndio wanakuwa katika madhara makubwa sababu sasa hivi kuna watoto wana keketwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara. Na niseme kwakuwa na dawati hili katika mkoa wetu watu watakuwa na nafasi ya kuja kuripoti Matukio yao katika haya madawati.”

Naye Kamishna wa polisi Faustine Shilogile, ambaye pia ni kamishna wa kamisheni ya polisi jamii ambayo madawati yote ya kijinsia yapo chini yake anasema madawati haya yapo katika mikoa 35 ya kipolisi nchini Tanzania na yamekuwa msaada mkubwa katika utendaji kazi wao.

“Kupitia madawati haya na kuwa na ofisi zenye mazingira mazuri kama haya ambayo yanawezesha waathirika kuweza kuhojiwa na kutoa taarifa zilizo kamilika kwakweli tunashukuru sana. Tunawashukuru sana UNFPA na tunawaomba waendelee kutoa misaada ya namna hii kutoa ujenzi wa madawati

Naye Warren Bright ambaye ni Meneja Mawasiliano wa UNFPA nchini Tanzania anasema wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanatimiza malengo 17 ya Maendeleo Endelevu SDGs na jamii kuwa na ustawi bora.